Ajenda halmashauri mpya yatawala watia nia Katoro

GEITA: AJENDA ya kuanzishwa kwa halmashauri mpya katika jimbo jipya la Katoro wilayani Geita imeonekena kutawala sera za watia nia wa nafasi ya ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katoro kwa sasa ni Mamlaka ya Mji Mdogo lakini imeonekana kuwa kituo kikuu cha biashara za jumla na rejareja mkoani Geita hali iliyochochea ongezeko kubwa la wahamiaji na wakazi katika eneo hilo.
Wakinadi sera zao Agosti 03, 2025 mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM ngazi ya kata, watia nia watano waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM Taifa wameshadadia ajenda ya Katoro kupewa hadhi ya halmashauri.

Akizungumza na wajumbe wa kata ya Ludete na Katoro, mtia nia wa CCM, Mhandisi Kija Ntemi ameahidi iwapo atapewa ridhaa ya kugombea na kuwa mbunge wa jimbo hilo atasimamia maono hayo yatimie.
Mhandisi Ntemi amesema baada ya Katoro kuwa Jimbo, bado kuna kila sababu ya kuanzisha halmashauri ya Katoro ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma halmashauri ya Geita.
Amesema hoja ya Katoro kuwa halmashauri ni maono yenye kuwezesha huduma stahiki za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wakazi wa mji huo wa kibiashara ili kuchagiza uzalishaji na ukusanyaji mapato.

Amesema uwepo wa ofisi za halmashauri ya Katoro itapunguza changamoto ya miundombinu ya umeme, maji, barabara na kusogeza huduma stahiki za kiserikali ili Katoro iwe kitovu cha uchumi wa Geita.
Mbunge wa Busanda anayemaliza muda wake, Mhandisi Tumaini Magesa akinadi sera zake amekiri kuwa baada kupata jimbo la Katoro kutoka jimbo mama la Busanda bado kuna haja ya kupata halamshauri.
Aidha mtia nia mwingine ambaye ni Ester James amesema mbali na hitaji la ofisi za halmashauri amejipanga kuwekeza zaidi katika ofisi ya mbunge ili kuweka mahusiano kati ya viongozi na wananchi.

Kwa upande wake Wakili Saimon Malando ameongeza kuwa Katoro ni jimbo linalokua kwa kasi na hivo linahitaji huduma za karibu za viongozi na maofisa wa serikali kufanikisha maendeleo endelevu.
Naye Mathias Lupuga amesema mwakilishi bora wa wananchi ndiye anayeweza kubadili uchumi wa mtu mmoja mmoja na Kaoro kwa ujumla na kujenga Katoro iliyo bora leo na kesho kwa maslahi ya wote.



