JESHI la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Masanja Mihayo (31) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Ikandilo, Wilaya ya Geita kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake, Mihayo Masanja (10) kisha kuuzika mwili wake kwenye shamba la mahindi na pamba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo alibainisha hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari na kueleza tukio hilo ni la Oktoba, 2024 ndani ya Pori la Akiba, Kata ya Nyaruyeye, Tarafa ya Busanda wilayani Geita.
Jongo alisema tukio hilo lilibainika Januari 09, 2025 baada ya mama mzazi wa watoto hao kutaka kuwaona watoto wake bila mafanikio.
Alisema mama alipokosa ushirikiano kutoka kwa mzazi mwenzake alitoa taarifa polisi ambao walimsaka na kumkamata mtuhumiwa ambaye alihojiwa na kisha kukiri kumuua mtoto wake.
Alisema mtuhumiwa aliwaongoza na kuwapeleka Polisi mahali alipouzika mwili huo na taratibu za kisheria za kufukua mwili zilifanyika.
Alisema uchunguzi umebaini mtoto huyo alishambuliwa kichwani na sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia kipande cha mti wakati akiadhibiwa na baba yake mzazi na kusababisha kuvimba mwili wote.
“Imeelezwa baba mzazi alipoamka asubuhi alikuta mtoto huyo amefariki na kuamua kuuzika mwili huo kwenye shamba la mahindi na pamba.
“Kabla ya tukio la mauaji Oktoba 2024 mtoto huyo na mdogo wake mwenye miaka tisa (jina linahifadhiwa) waliondoka pori la akiba ili waende Katoro kwa mama yao mzazi aitwaye, Joyce Andrew lakini hawakufanikiwa kwani baba yao aliwarejesha.
“Kutokana na tabia hiyo, mtuhumiwa alichukizwa na kitendo cha watoto hao kutoroka na kwenda kwa mama yao, hivyo aliamua kumuadhibu mtoto wake mkubwa ili asirudie tabia hiyo,” alieleza Kamanda.
Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani