Anaswa akijaribu kumhonga ofisa Takukuru

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imemtia mbaroni Suleiman Mwishehe na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kujaribu kumhonga ofisa wa taasisi hiyo aliyekuwa anachunguza tuhuma dhidi ya ubadhilifu wa Sh milioni 90 .

Fedha hizo ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu na vyumba vya madarasa ya shule ya msingi katika kijiji cha Mlilingwa, kata ya Tununguo, Wilaya ya Morogoro

Mkuu wa taasisi hiyo mkoani humo, Manyama Tungaraza ametoa taarifa hiyo leo Februari 5, 2024 mjini Morogoro katika taarifa ya kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023 cha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo ufuatiliaji na utekelezaji miradi ya maendeleo inayohusu elimu, maji na mifugo.

Mwishehe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi na Mlezi wa Kikundi cha Bosu Kuku Group, alikamatwa  baada ya kumpa ofisa wa Takukuru kiasi cha Sh milioni 3 kati ya 5 alizoshawishi awali kuwa yeye (Mwishehe) na watuhumiwa wenzake watampa ili wasifikishwe mahakamani .

Tungaraza amesema  mtuhumiwa huyo alipofikishwa mahakamani alikiri kosa na kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 500,000 na fedha alizozitoa kama hongo kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Mkuu wa Takukuru mkoa amesema mshitakiwa alilipa faini ya Sh 500,000 na  kiasi cha Sh milioni 3 zilitaifishwa na kuwa za serikali.

Ametoa onyo kwa mwananchi yoyote asijaribu kushawishi au kutoa hongo kwa mtumishi wa Takukuru mahali popote mkoani humo kwa lengo la kuharibu uchunguzi au ushahidi wa tuhuma zozote zinazochunguzwa na Takukuru kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Tungaraza ameelezea  mazingira ya kukamatwa kwa Mwishehe kuwa  baada ya kuidhinishiwa kwa mradi huo na thamani ya Sh milioni 90  ambazo zilipitia kwake alikaa nazo muda mrefu bila kuanza kuifanya kazi hiyo.

Mkuu wa Takukuru mkoa amesema baada ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano na kuhojiwa alioana sio sawa na kwamba ataweza kufikishwa mahakamani.

“Alipogundua alianza kushawishi kuwa atatoa sh Sh milioni tano ili suala hilo lisiende Mahakamani na taarifa zake kupatikana tukamwambia ofisa wetu amwambie alete hizo fedha naye alizileta fedha hizo hapa  ofisimi kwetu Takukuru mkoa na akakamatwa hapa kwetu na fedha zake Sh milioni 3.” amesema Tungaraza .

 

Habari Zifananazo

Back to top button