Anayedaiwa kuchoma nyumba iliyoua mama, watoto 4 akamatwa

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limewakamata watu wawili akiwemo Mwita Chacha aliyekuwa anatafutwa kwa tuhuma za kuchoma nyumba moto na kusababisha vifo vya watu wanne ambao ni mama na watoto wake watatu.
Mtuhumiwa mwingine ni Hamisi Hamisi (21) aliyekamatwa na mali ya wizi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi alisema Mwita alitekeleza mauaji hayo kutokana na madai ya kuwa familia ya marehemu ilimpa sumu mtoto wake.
“Tumefanikiwa kumkamata Mwita Chacha aliyekuwa anatafutwa kwa tuhuma za kuchoma nyumba moto katika Kijiji cha Manga Wilaya ya Handeni,” alisema.
Aliongeza: “Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wanne wakiwemo, mama Pili Saguge na watoto wake watatu ambao ni Chacha Nyabilenga, Jane Nyabilenga pamoja na Makabala Nyabilenga.”
“Mwita Chacha alikamatwa akiwa amejificha jijini Mwanza na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yake,” alisema Mchunguzi.
Katika tukio la pili, Mchunguzi alisema Januari 6, 2025 saa 8:30 mchana, jeshi la polisi lilimkamata Hamisi ambaye ni mkazi wa Majani Mapana jijini Tanga.
Alikamatwa na mali ya wizi ambayo ni vitu mbalimbali vilivyoibwa baada ya nyumba moja ya mwananchi kuvunjwa Desemba 16, 2024 katika eneo la Uzunguni.
Mchunguzi alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na na bastola moja aina ya Kevin-ZVI yenye namba H06403 magazini mbili za bastola bila ya risasi, kompyuta mpakato mbili aina ya Macbook Air na MacBook Pro, saa sita za mkononi, sime moja, shanga moja ya kiunoni na sabuni tatu za kuogea ambavyo ni vitu vilivyoibiwa.



