ASAS awahamasisha wana Kilolo kuweka rekodi Oktoba 29

Mratibu wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, amewataka wana CCM na wananchi wa jimbo la Kilolo na mkoa mzima wa Iringa kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani, ili kuendeleza kasi ya maendeleo iliyoanzishwa katika miaka mitano iliyopita.
Akizungumza wakati akizindua kampeni za jimbo la Kilolo na kumnadi Ritta Kabati, mgombea ubunge wa CCM wa jimbo hilo, Asas alisema hatua kubwa za maendeleo zilizotekelezwa na serikali ya CCM ni ushahidi tosha wa sababu za wananchi kuendeleza uongozi huo.
“Asilimia kubwa ya wana Kilolo wanashuhudia mafanikio haya. Ni wajibu wetu kuendelea kuyatetea kwa kuhakikisha tunachagua mafiga matatu Rais, mbunge na madiwani,” alisema Asas.

Akiainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika wilaya ya Kilolo pekee, Asas alisema serikali ya CCM imeongeza vituo vya afya na zahanati 10, imejenga madarasa 495, vyoo 352, na maabara tisa katika shule za sekondari na msingi.
Aidha, shule mpya 20 za msingi na sekondari zimeanzishwa, miradi mikubwa ya maji imefanyika katika maeneo ya Ilula, Mlafu na Mahenge, huku ujenzi wa daraja la Ruaha Mbuyuni–Msasa na maegesho ya magari ukiendelea.
Mradi wa ujenzi wa sekondari ya wasichana Lugalo wenye thamani ya Sh bilioni 5, barabara ya Ipogolo–Kilolo yenye thamani ya Sh bilioni 65, pamoja na skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni yenye thamani ya Sh bilioni 4, ni miongoni mwa miradi mikubwa inayoshuhudia mageuzi makubwa ya miundombinu katika jimbo hilo.
“Asiyejua kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk Samia na Serikali ya CCM ni kwa sababu ya hulka ya kupotosha ukweli,” alisisitiza Asas.

Kuhusu mgombea ubunge Ritta Kabati, Asas alisema anamfahamu kwa zaidi ya miaka 15 na ameshiriki naye katika miradi ya kijamii, hasa kusaidia watu wenye ulemavu na kuboresha sekta ya afya.
“Ritta ana uzoefu wa miaka 15 bungeni akiwa mbunge wa viti maalum. Haendi bungeni kushangaa, anajua kazi yake na ana uchungu wa wananchi wa Kilolo,” alisema Asas, akisisitiza kuwa Kabati ataanza kazi mara moja bila kusubiri maelekezo.
Kwa upande wake, Ritta Kabati aliwahakikishia wakazi wa Kilolo kuwa yeye si mgeni katika siasa za jimbo hilo kwani amefanya kazi kwa karibu na wabunge watatu waliomtangulia, akijua vyema changamoto zinazolikabili.
Aliahidi kufanyia haki Ilani ya CCM na kueleza kuwa barabara zitakuwa kipaumbele chake cha kwanza mara baada ya kuapishwa.

“Kilolo ina utajiri mkubwa na kata nyingi. Umoja, upendo na mshikamano ndio utakaotuvusha kimaendeleo. Wanawake tunaweza kubeba mizigo, akina baba watuamini,” alisema Kabati.
Alitoa wito kwa wananchi wote wa jimbo la Kilolo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuunga mkono wagombea wote wa CCM ili “mafiga matatu”—Rais, mbunge na madiwani—yaendelee kuleta mabadiliko ya kweli.



