Asilimia 30 zabuni za umma zatengwa makundi maalumu

IRINGA: Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mifumo rasmi ya uchumi kwa kuchangamkia fursa ya asilimia 30 ya zabuni za umma, ambazo zimetengwa mahsusi kwa makundi hayo kupitia Sheria ya Manunuzi ya Umma, Sura 410.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felista Mdemu, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa maafisa maendeleo ya jamii wa ngazi ya kata hadi mkoa kutoka mkoani Iringa.

Mafunzo hayo yameandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), kwa lengo la kuwawezesha maafisa hao kujua kwa kina namna ya kusaidia makundi maalum kunufaika na zabuni hizo kupitia mifumo rasmi ya manunuzi ya umma.

“Serikali imefungua milango. Tunahitaji kuona maafisa maendeleo ya jamii wakisimama imara kama walimu na washauri wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujisajili,” alisema Mdemu.

Alisema fursa hizo haziwezi kutumika kikamilifu iwapo jamii haitafikiwa kwa wakati kupitia wataalamu waliopo ngazi za halmashauri, kata na vijiji.

“Katika mkoa wa Iringa kuna vikundi 12 tu wakati Mbeya wana 29. Tengenezeni vikundi vipya, hamasisheni ushiriki wa makundi haya,” alisema Mdemu.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii nchini, Patrick Golwike, alifafanua kuwa makundi hayo yamekuwa yakikosa zabuni si kwa sababu ya ukosefu wa fursa, bali kwa kukosa maandalizi ya msingi.

“Tunasisitiza nidhamu ya kibiashara, utayari na uelewa wa taratibu za zabuni. Wizara itaendelea kutoa elimu kupitia semina, warsha na kampeni za kitaifa ili kuhakikisha kila anayestahili ananufaika,” alisema.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde, alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali kuwajengea uwezo maafisa maendeleo ya jamii ili waweze kuongoza jitihada za kuhamasisha uundwaji wa vikundi vipya na kuviunganisha na mifumo rasmi ya uchumi.

Kwa ujumla alisema mafunzo hayo yanachochea ari kwa maafisa maendeleo ya jamii kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo yao, kwa kuhakikisha makundi maalum yanajitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za zabuni zinazotolewa na taasisi za umma, kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kushiriki moja kwa moja kwenye ujenzi wa taifa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, aliyehudumu kama Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi, alipata mafanikio makubwa katika kuingiza makundi maalum katika mfumo rasmi wa uchumi.

Akitoa mfano wa mafanikio hayo alieleza jinsi halmashauri ya Bahi ilivyoweza kuyahusisha makundi haya kupitia utoaji wa mikopo na fursa za kushindania zabuni.

Alisema katika halmashauri hiyo ya Bahi, mafundi seremala waliokuwa kwenye vikundi rasmi walipewa tenda kutengeneza milango, madawati, meza na viti kwa katumizi ya shule mbalimbali.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yamewezeshwa na ushirikiano wa karibu kati ya idara ya maendeleo ya jamii na manunuzi, ambapo vikundi hivyo vilisajiliwa kwenye mfumo wa NeST.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Venance Ntyarundula, aliyetoa salamu kwa niaba ya uongozi wa mkoa, alisema kuwa mkoa umeazimia kufanya kongamano la kila mwaka la maafisa maendeleo ya jamii ili kutathmini changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa sera zinazolenga kuinua maisha ya wananchi.

“Mwaka huu wa fedha tunaanza tofauti. Pale ambapo vikundi vitapewa tenda, vitapata mapato na uchumi wao utabadilika. Mpango huu unahakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma,” alisema Ntyarundula.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button