Asilimia 99.31 wakutwa salama mikesha ya mwenge Geita

MKOA wa Geita umeweka wazi kuwa katika mikesha ya mwenge wa uhuru kuanzia Septemba 01 hadi 07 takribani asilimia 99.31 ya watu waliopima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) wamekutwa salama.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigella ametoa takwimu hizo Septemba 08, 2025 wakati akikabidhi Mwenge wa uhuru kwa mkoa wa Kagera baada ya kuhitimisha mbio zake zilizoanza Septemba 01 hadi 07, 2025 mkoani Geita.
Shigella amesema katika mikesha ya Mwenge wa uhuru mwaka 2025 wananchi waliojitokeza kupima Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) walikuwa 2,298 na kati yao wanaume 1,522 na wanawake 776.
Amesema matokeo ya vipimo vya VVU yanaonyesha wananchi waliokutwa na maambukizi ya VVU walikuwa 16 pekee sawa na asilimia 0.69 ambapo wanaume ni 11 na wanawake ni watano.
Amesema kwa upande mwingine jumla ya wananchi waliojitokeza kupima malaria, walikuwa ni 920, na waliokutwa na vimelea vya malaria ni 52 sawa na asilimia 5.6, kati yao wanawake ni 34 na wanaume 18.
Shigella amesema matokeo hayo yanadhihirisha mwitikio chanya kwa watanzania kushirikiana na serikali katika kuunga mkono kampeni ya kupiga vita VVU, malaria.
Ameongeza kuwa katika kuunga mkono kampeni ya upandaji miti, katika mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 kampeni imewezesha upandaji miti takribani 1,628,231 kwa halmashauri zote za mkoa wa Geita.
Amesema katika kuhamasisha nishati safi, Mwenge wa Uhuru umetembelea miradi 13 na kugawa mitungi ya gesi ya kupikia 3,957 kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.



