Askofu kanisa la ufunuo Shinyanga ahubiri amani

SHINYANGA: ASKOFU wa Kanisa la Ufunuo mkoani Shinyanga, Samawi Bendera amewashauri waumini wa kanisa hilo kujiepusha na vurugu kwani kuna baadhi ya nchi watu wake wamekuwa wakiingia kanisani kuhubiri kwa hofu kutokana na kukosa amani.
Bendera ameeleza hayo Januari 2, akihubiri kanisani kwake wakati wa ibada maalumu ya kuliombea taifa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kumshukuru mungu kwa kuingia mwaka 2026 wakiwa na afya njema huku mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda.
Bendera amesema kanisa hilo tangu kuanzishwa kwake limekuwa likiendesha ibada zake kwa kuhakikisha amani inakuwepo na leo ibada hii maalum inawaeleza waumini wake nchi ikivurugika hakuna masikini wala tajiri wote wataathirika kwa vurugu zitakazo tokea.

“Upendo sio kuunga mkono maneno yenye kuleta vurugu sisi tunahubiri kwa amani, nendeni nchi za wenzetu kama Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Sudani Kusini wanahubiri wakiwa na hofu hivyo waumini muwe mabalozi wazuri wa amani ya nchi,”amesema Bendera.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda katika ibada hiyo maalumu ya kuliombea taifa amesema kuna mamlaka mbili ya kimwili na kiroho na yote yanatakiwa kuvungamana pamoja ili kuwepo na amani kwa wananchi wake.
Nkinda amesema uzalendo katika taifa unahitajika kwani hata kwenye kitabu cha dini (Biblia ) watu wake zamani walionyesha kutokata tamaa sababu ya changamoto zilizokuwepo hivyo watambue dunia inaongozwa kiroho na serikali inaongoza kimwili hivyo dini inatakiwa isimame sana katika jamii na viongozi wake wasijisahau kuhubiri.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama Thomas Myonga amesema vurugu zilifanywa na baadhi ya vijana walikuwa wakifikiri ndiyo mwisho wa maisha yao hali ambayo imewafanya waendelee kuishi maeneo hayo na kukosa ofisi muhimu walizokuwa wakizitegemea kutoa huduma.

“Jamani wazazi tusiichekee vita kwani tukiwa na watoto wanasoma ndiyo unakuwa mwisho wao wa kupata elimu, kama wa kike hawataolewa wataishia kubakwa na wakiume kulawitiwa hali ya kukaa ndani hatukuzoea hivyo tuilinde amani ya nchi yetu kwa nguvu zote,”amesema Myonga.
Myonga amesema nchi ya Tanzania hailwindi kwa kutumia bunduki bali imekuwa ikilindwa siku zote na madhehebu ya dini ambayo yalikuwa yakichangia jamii kumjua mungu maana nchi ilitengenezwa kwa amani na utulivu tangu ilipopata uhuru wake.



