Atoa Sh elfu tano kumpongeza Rais Samia

MLELE, KATAVI; Aseni Jandikile mkazi wa Kijiji cha Luchima  Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ametoa Sh elfu tano kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Kiasi hicho cha pesa kimekabidhiwa kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda Mei 03, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Luchima wakati wa ziara yake ya kuwafariji wananchi waliopatwa na mafuriko katika jimbo la Kavuu.

‘’Nampongeza Rais Samia kwa vitendo kabisa naomba mhe, mbunge leo nikukabidhi fedha taslimu shilingi elfu tano umpelelekee Mhe, Rais ’’ alisema Jandikile.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, uamuzi wake unatokana na kuwiwa na uongozi bora na utendaji kazi wa Rais Samia hasa kwa kuwajali wananchi wa Luchima ambapo mbali na mambo mengine amewajali kwa kutoa fedha Sh milioni 50  kwa ajili ya ujenzi wa zahanati aliyoieleza imewakomboa wananchi wa kijiji hicho.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda amesema atahakikisha kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na mwananchi huyo kinamfikia Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Amempongeza mwananchi huyo wa kijiji cha Luchima wa uamuzi wake wa kutoa kiasi hicho cha fedha kama ishara ya kukubali juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia.

Habari Zifananazo

Back to top button