Auawa akidaiwa kufumaniwa na mke wa mtu

MWANZA: MGOCHI Herman ,29, mwendesha bodaboda mkazi wa Kitangiri jijini Mwanza amekutwa amekufa baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake huku chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni alifumaniwa akiwa amelala na mke wa mtu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo linadaiwa kufanywa na Athman Morandi Stanslaus ,36, dereva na mkazi wa mtaa wa Ghana, Ilemela jijini humo.
Kamanda Mutafungwa amesema kuwa Athman, ambaye tayari anashikiliwa na polisi anatuhumiwa kumuua Herman baada ya kumfumania akiwa na mke wake ndani ya chumba chake.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amewatakia wakazi wa Mwanza heri ya Sikukuu ya Eid El-Fitr na kuwasihi kuisherehekea kwa amani na utulivu.



