KAMATI ya Siasa Mkoa wa Arusha imeiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kurekebisha mifumo ya maji ili kuwezesha upatikanaji wa maji kwenye mabweni mawili ya wanafunzi shule ya sekondari Mringa iliyojengwa kwa Sh milioni 260.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Arusha, Loy Thomas ole Sabaya wakati wa ukaguzi wa hali ya mradi wa ujenzi wa mabweni mawili ya miundombinu ya sekondari nchini (SEQUIP).
Wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao umeongeza ari ya watoto wa kike kusoma kwenye mazingira salama chini ya uangalizi wa walimu na kumwagiza Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Injiani Justine Rujomba kurekebisha mfumo wa maji shuleni hapo na kuhakikisha maji yanatoka shuleni hapo muda wote.
“Ondoeni changamoto ya tatizo la maji shuleni hapa, maji yatoke siku zote, hapa kuna wanafunzi wengi hivyo uwepo wa maji ya uhakika ni muhimu, ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na wanafunzi kutumia muda mwingi kusoma badala ya kwenda kutafuta maji na ndoo kichwani”.
Hata hivyo Sabaya pia ameipongeza serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Arusha kwa mradi huo unanufaisha wanafunzi zaidi ya 2,551,lakini pia walimu wanaofundisha shule hiyo ambao hawakupenda kutaja majina yao waliiomba serikali kuwasaidia kuongeza matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu sanjari na ofisi nzuri ya walimu tofauti ya sasa ambayo ni finyu
Awali, wajumbe wa kamati hiyo, wamefanya ziara ya kawaida ya siku mbili ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, ikiwa ni ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM katika Halmashauri ya Arusha, Wilaya ya Arumeru.