Aweso ataka utekelezaji maagizo ya Rais Samia

DAR ES SALAAM: Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesisitiza Mamlaka za Maji nchini ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufunga mita za malipo ya kabla kwa wateja kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote.

Ametoa wito huo wakati wa hafla ya futari ya DAWASA na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, Viongozi wa Mkoa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wadau wengine wa Sekta ya Maji iliyoenda sambamba na dua maalum ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa agizo hilo, wizara itashirikiana na Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha utekelezaji wa agizo hili unafanyika vizuri.

Aidha, Aweso ameitaka DAWASA kuongeza nguvu katika kukabiliana na upotevu wa maji kwenye maeneo yote ya huduma ili kuimarisha usambazaji wa maji kwa wateja wote.

Ameipongeza Mamlaka kwa kuendelea na utekelezaji mzuri wa majukumu yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kuahidi wizara kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa ili huduma ya majisafi iweze kuwafikia wote sambamba na malengo ya serikali ya kusambaza maji mijini kwa asilimia 95 na vijijini kwa asilimia 85 kufikia mwaka 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameipongeza Serikali kwa jitihada zinazofanyika za kuhakikisha huduma ya maji inafika kwa kila mwananchi.

Habari Zifananazo

Back to top button