Baba aua kichanga wa miezi mitano kwa kumpiga na kiatu, mkanda

GEITA: MWANAUME mmoja mkazi wa mtaa wa Kilimahewa, Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita, Kubilu Mahege (20) amemuua kwa kumpiga mwanaye mchanga kutokana na ugomvi wa kifamilia.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Safia Jongo amethibitisha tukio hilo na akieleza lilitokea Januari 11, 2024 majira ya saa saba usiku eneo lijulikanalo kama Kigamboni.
 
Kamanda Jongo amemtaja mtoto ambaye kwa sasa ni marehemu ni, Leonard Kubilu mwenye umri wa miezi mitano ambapo alifariki baada ya kupigwa kwa kutumia kiatu cha kike na mkanda na baba mzazi.
 
“Chanzo cha tukio hili ni ugomvi wa kifamilia na huyu baba alitoweka mara tu baada ya kufanya tukio hili lakini juhudi zinafanyika za kumtafuta mtuhumiwa.
 
“Kutokana na tukio hili nitoe wito kwa jamii kumrudia Mungu kwa sababu nikiangalia tukio kama hili hata kama kuna ugomvi, mtoto wa miezi mitano hajui hata kuongea alimkosea nini huyu baba.
 
“Kwa hiyo ni kama ni ugomvi kati ya mama na baba, sasa inakuaje ugomvi wa baba na mama unapelekea machungu kwa mtoto, mtoto anahusika na nini.” Amesema Kamanda Jongo.

Habari Zifananazo

Back to top button