‘Bahari Accelerator’ kubadili tafiti za bahari kuwa biashara

DAR ES SALAAM; WADAU wa uchumi wa buluu ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), wamekutana Dar es Salaam kujadili masuala ya uchumi huo na kuzindua mradi wa Bahari Accelerator wenye lengo la kubadili tafiti za ubunifu kuwa biashara katika maeneo ya maji ya Tanzania yakiwemo maziwa na bahari.

Mkurugenzi Mkuu wa Tafiri Ismael Kimirei, amesema awamu ya kwanza ya mradi huo itatekelezwa kwa miaka mitatu ikiwa na lengo la kufanyia kazi utafiti wenye ubunifu na kuwezesha wabunifu wake kubadili tafiti hizo kuwa bidhaa za biashara kwenye sekta ya bahari.

“Tutakuwa tunachukua matokeo ya utafiti ambayo ni bunifu, kuyawekea msingi wa wale watafiti kwanza kulinda haki za mwingiliano wa kazi, kuwakuza kwa maana ya kuwajengea uwezo na kuwajengea uwezo wa kutoka kwenye kubuni mpaka kuwapeleka kwenye kuzalisha bidhaa kutokana na utafiti wao. Kazi kubwa tutakayofanya itakuwa ni hiyo kuwainua watafiti kufikia hatua hiyo,” amesema Kimirei.

Amesema Tafiri kwa kushirikiana na wadau itawasaidia watafiti wabunifu kuhakikisha kazi wanazofanya kwenye uchumi wa bluu zinatekelezeka kwa kuwatoa kwenye wazo kwenda kwenye kuzalisha bidhaa kama biashara.

“Tutashirikiana na wadau kutafuta mitaji, kwa sababu unaweza kuwa na wazo lakini ukakosa hela likafa na sisi hatutaki Mawazo yao yafe kwa sababu wabunifu hawa wana hitaji kujengwa, kukuzwa ili tuweze kutengeneza ajira na kuisaidia nchi yetu,” amesema Kimerei.

Amesema Tafiri kwa sasa inatafuta mtaji wa dola za Marekani milioni 1.2 kwa utekelezaji wa mradi huo.

Awali baada ya kuzindua Mkutano huo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti alisema
sekta ya uchumi wa bluu ni fursa ambayo ilikuwa haijatiliwa mkazo, lakini kwa sasa serikali kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka nguvu kubwa sana kwenye uchumi wa bluu, kwa kutoa elimu kwa wananchi ambayo itawasaidia kufahamu nini kilichopo kwenye uchumi wa bluu.

Amesema tayari Rais Samia amenonesha njia kwa uwezeshaji wa mikopo na kuhamasisha watu wawekeze katika sekta ya Bahari ikiwa ni pamoja na kilimo cha mwani, ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na kutoa boti za kuwezesha wavuvi kufika kwenye maji ya kina kirefu.

Pia amesema jamii bado haijatumia vizuri rasilimali za Bahari kujipatia manufaa ya kiuchumi hivyo umefika wakati rasilimali hizo zitumike ipassavyo zote kwa pamoja.

Meneja wa taasisi inaypjishughulisha na uhifadhi wa mazingira duniani ya IUCN, Elinasi Monga ameema mkutano huo unakutanisha watafiti, watunga sera na wafanyabiashara wa masuala ya uchumi wa bluu ukiwa na lengo kuunganisha nguvu kuinua sekta hiyo ili inufaishe wadau wote.

“Kwa kipindi kirefu, kwa miaka mingi watu ambao wanafanya utafiti wamekuwa wakifanya utafiti wenyewe, wanaofanya biashara wanafanya wenyewe na watunga sera za uchumi wa bluu na masuala ya bahari wamekuwa wakifanya kazi wenyewe kwa hiyo mkutano huu unawaleta pamoja kuangalia jinsi gani tafiti zinaweza kusaidia kuandaa na kutekeleza sera lakini pia jinsi gani tafiti zinaweza kuboresha biashara ya uchumi wa bluu,” amesema Monga.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button