BAKWATA Katavi waja kidigitali

KATAVI; Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Katavi, limezindua mfumo wa matumizi ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali za kiofisi.
Katavi unakuwa mkoa wa kwanza nchini Tanzania kuanza kutumia mfumo huo tangu kuzinduliwa na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakary Zubeir.
Akizindua mfumo huo Meneja wa Benki ya TCB, Chacha Petri amepongeza hatua hiyo ya BAKWATA kuingia kwenye matumizi ya TEHEMA na kueleza kuwa huo ndio mfumo wa kisasa ambao taasisi makini inapaswa kuutumia.

Katika hatua nyingine Chacha ameahidi kutoa vifaa ikiwemo kamera na kompyuta mpakato (laptop) kwa BAKWATA Mkoa wa Katavi kama moja ya njia ya kuendalea kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwa taasisi hiyo.
Sheikh wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu amesema mfumo wa TEHAMA ni moja kati ya hatua za mabadiliko ndani ya BAKWATA chini ya Mufti Zubeir wa kutaka Waislam kutoachwa nyuma na teknolojia.
Uzinduzi wa mfumo huo umejumuisha ugawaji wa vishikwambi vinne, ambavyo vitasaidia kuendesha mfumo wa TEHAMA katika ofisi ya BAKWATA Mkoa wa Katavi, Ofisi 3 za BAKWATA Wilaya za Mpanda, Tanganyika na Mlele na printa moja kwa ajili ya ofisi ya mkoa.



