Bakwata: Tambueni thamani ya kura zenu

DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Shekhe Alhaj Nuru Mruma, amewataka Watanzania kutambua thamani ya kura zao kwa kusisitiza kuwa kura moja inaweza kumuweka madarakani kiongozi asiye sahihi.

Akizungumza na Daily News Digital jijini Dar es Salaam, Shekhe Mruma amesema ni muhimu kuondoa dhana potofu kwamba kuna watu maalumu wa kufanya maamuzi ya nani awe kiongozi, akibainisha kuwa kila raia ana mchango mkubwa kupitia kura yake.

Aidha, Shekhe Mruma amesema rushwa imekuwa ikiharibu mchakato wa uchaguzi kwa kuwa inaathiri maamuzi ya wapiga kura, ambapo amesema viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa hukosa uadilifu na hushindwa kutekeleza sera zenye tija kwa wananchi, tofauti na kuongozi ambaye atachaguliwa kutokana na uzuri wake wa sera, uwezo wake na kwa uadilifu wake.

Katika hatua nyingine, Shekhe Mruma amesema mapungufu yaliyopo katika siasa hayawezi kuzuia uchaguzi kuwa huru na wa haki, lakini yanapaswa kushughulikiwa mapema ili yasivuruge amani na haki ya wananchi kushiriki uchaguzi.

Amezisihi mamlaka zinazohusika na uchaguzi kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu na kwamba dosari zilizopo katika mifumo ya uchaguzi zinarekebishwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Pia amezishuri mamlaka hizo kutoa elimu ya kutosha ya uchaguzi kwa wananchi wote ili kila mmoja aelewe nafasi na wajibu wake, na kwa kufanya hivyo kutaepusha migogoro isiyo ya lazima.

“Tujiandae kuingia katika uchaguzi na tutegemee kuwa uchaguzi utakuwa na amani, na tutapata viongozi ambao watakuwa na mustakabali mzima wa kutuongoza katika miaka hii mitano ijayo” amesema Shekhe Mruma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button