Bakwata yakemea upandishaji bei bidhaa kwenye mfungo

DODOMA; MWENYEKITI wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Dodoma, Bashiru Omary amewataka wafanyabiashara kutotumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kama sehemu ya fursa ya kupandisha bidhaa zao kwa wateja wao.

Alitoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma jana, huku akiwataka wafanyabiashara kuelekea Ramadhani kujiepusha na upandishaji wa bei wa bidhaa zao.

Alisema kuwa wakifanya hivyo watakuwa wanawaumiza wateja wao kiuchumi. “Hata kiongozi wetu Mtume Muhammad (S.A.W) mwenyewe ameonya tabia kama hiyo ya kupandisha bidhaa kwa njia ya dhuluma,” alisema.

Alisema mfungo wa Ramadhani si wote ambao wana kipato cha kuwawezesha katika kujikimu kimaisha ya kila siku, hivyo kitendo cha kupandisha bidhaa kinaweza kuwaumiza na kikawanyima haki ya kufunga kama wengine.

“Kimsingi kitendo cha kupata faida kwa njia udhalimu isiyo halali kiungwana na siyo jambo jema mbele ya Mwenyezi Mungu, ukizingatia kuwa mwezi huo wa mfungo ni wa toba pamoja na kuwasaidia wale watakaonekana hawajiwezi kiuchumi,” alisema.

Aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha katika kipindi hicho cha mfungo kudumisha amani iliyopo pamoja na kuiombea nchi, rais na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu uwe wa haki na uwazi.

Aidha, amewakumbusha waumini wenye kipato cha juu katika kuelekea kwenye mfungo huo wa Ramadhani kuwakumbuka wenye uhitaji na wasiojiweza kiuchumi ikiwemo wajane, yatima, wazee wanaoishi katika mazingira magumu na watoto wanaolelewa kwenye vituo.

Aliwataka viongozi wa dini ndani ya misikiti kutumia majengo hayo kuhakikisha waumini wanafanya ibada ya kuombea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, ikiwa na pamoja kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Alisema kuwa Watanzania wanahitaji amani iendelee kuwepo, hivyo wajibu wa kuomba na kulinda upo mikononi mwa kila mmoja na si vinginevyo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button