Bakwata yatahadharisha chuki, visasi uchaguzi mkuu 2025

DODOMA :BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Dodoma limevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu viimarishe umoja badala ya kuwekeana visasi, chuki na uadui. Pia, Bakwata Dodoma imehimiza wagombea katika nafasi zote wafanye kampeni kwa kuzingatia amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Dk Mustaph Rajabu alisema hayo jijini Dodoma wakati wa ibada ya swala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Gadaffi. Dk Rajabu alihimiza wagombea waondoe tofauti zao za kisiasa kwa kuwa zinaweza kusababisha nchi kuwa na makundi na kuwekeana visasi na chuki. Alisema ni muhimu kuwe na umoja ndani ya vyama vya siasa na nje ya chama kimoja hadi kingine ili kulinda amani ya nchi.
“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, kwa maana hiyo vyama vya siasa navyo vinatakiwa kuwa kitu kimoja na kuimarisha amani iliyopo badala ya kuwekeana visasi na chuki kutokana na utofauti wa vyama vya siasa,” alisema.
Shehe Rajabu pia aliwataka Watanzania waepuke kujiingiza kwenye uchaguzi kwa kuchagua viongozi wabovu kutokana na vishawishi vinavyoweza kutolewa ili wagombea hao wachaguliwe. Mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Dodoma, Bashiru Omary aliwataka mashehe wa misikiti kutofanya shughuli zao kwa kutaka kuongozwa kwa kila jambo, wasimame kwenye nafasi zao kiutendaji.
Omary alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wasimamizi ndani ya misikiti wanaofanya kazi kwa mazoea na kwa kutaka kusimamiwa kwenye nafasi zao. SOMA: Waratibu INEC wapewa neno makundi Whatsapp
“Niwaombe viongozi mlioaminiwa na umma wa dini ya Kiislamu fanyeni kazi zenu kwa kujiamini na kwa kufuata miongozo ya imani ya dini yetu, niwaombe muache kufanya shughuli zetu kwa mazoea bali mnawapaswa kubadilika kwenye utendaji wenu,” alisema.



