Balozi, bosi Sonatrach wateta fursa za uwekezaji sekta ya mafuta, gesi asilia
Balozi Njalikali na mkuu huyo wa Sonatrach wateta fursa za uwekezaji sekta ya mafuta, gesi asilia

Algiers, Algeria: Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Iman Njalikai amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Algeria (Sonatrach), Rachid Hachichi kwa lengo la kujadili namna gani pande hizo mbili zinaweza kushirikiana katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.
Kupitia mkutano huo uliofanyika jijini Algiers Jumapili (Septemba 7, 2025) na kuwaleta pamoja viongozi na maafisa waandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) pamoja na wale wa Sonatrach, nchi hizo mbili pia ziliangazia fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi hizo mbili za Afrika.
Mazungumzo hayo yalifanyika Septemba 07, 2025 Jijini Algeris, Algeria na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Sonatrach na ujumbe wa watanzania uliojumuisha viongozi na maafisa waandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA)
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Iman alisema kuwa, ingawa Tanzania na Algeria zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika maeneo mbalimbali, ni kwa mara ya kwanza mazungumzo yanafanyika kwa kuihusisha Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli nchini (PURA)
“Ninafahamu kuwa Sonatrach na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) zilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) na kuziwezesha taasisi hizo kushirikiana kwa karibu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.
“Tunaishukuru Sonatrach kwa kuendelea kutufungulia milango na kwa hakika, tumeona matunda ya mashirikiano katika eneo hili,” aliongeza mwanadiplomasia huyo.
SOMA: PURA, ALNAFT wakutana Algiers kujadili namna ya kuinua sekta ya gesi asilia
Pamoja na shukrani hizo, Balozi Iman alisema kuwa, bado Tanzania inaendelea kujenga uwezo wa wataalamu wake wakiwemo wataalamu wanaofanya kazi PURA hivyo Sonatrach hivyo kuiomba Sonatrach kuendelea kutoa fursa za mafunzo na programu za kujenga uwezo.

Mwakilishi huyo wa Tanzania huko Algeria pia aliikaribisha Sonatrach kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania hususan katika vitalu vya utafutaji wa mafuta mara baada ya zoezi la kunadi vitalu kuzinduliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Sonatrach, Hachichi alisema kuwa Sonatrach ipo tayari kutumia fursa na kuendelea kushirikiana na taasisi za Tanzania ikiwemo PURA katika kujenga uwezo wa wataalamu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.



