Barabara kuifungua Tanga kibiashara, kiutalii

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Pangani -Saadani – Tanga inayojumuisha Daraja la Mto Pangani, itaufungua Mkoa wa Tanga kibiashara na kiutalii.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na wananchi wa Pangani mkoani Tanga baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 256 na daraja likiwa na urefu wa mita 525.
Rais Samia alisema kupitia barabara hiyo, eneo huru la kiuchumi linakwenda kujengwa ambalo pia litahusisha nchi jirani ya Kenya.
“Barabara hii tunayoiunganisha inakwenda kuifungua Tanga kiutalii na kibiashara. Pia maeneo kadhaa ya utalii, sehemu mbalimbali za Tanga ambazo hazifikiki kwa barabara hii ni rahisi kumtoa mtalii Saadani na kumpeleka maeneo mengine na kufanya utalii ndani ya Tanga,” alieleza Rais Samia.
Alisema mradi huo unaunganisha maeneo mengi kutoka Bagamoyo hadi mpaka na Kenya na kuwa kutokana na miundombinu kuwa rahisi, serikali itajenga kongani kubwa ya viwanda Bagamoyo.
“Pia tunaiunganisha Tanga tena kupitia Pangani, Pangani hii itaunganisha majimbo mengi ya Bagamoyo, Tanga na itakwenda moja kwa moja mpaka kwenye mpaka wetu na Mombasa ambako Mombasa kule nadhani kwa kupitia mfadhili huyuhuyu na wenyewe wanajenga kuelekea mbele na kutuunganisha na Bandari ya Mombasa,” alifafanua Rais Samia.
Alisema barabara hiyo pia itaunganisha na Pwani ya Afrika Mashariki kwani baada ya kutoka mpaka wa Horohoro na kupita Tanga, Bagamoyo na kufika Dar es Salaam na kufanya urahisi wa kufika Mtwara na Lindi.
“Naambiwa kwamba Pangani hapa ni wakulima wazuri wa mkonge, mihogo na nazi, sasa hii barabara inakwenda kutafuta biashara na pengine kuwavutia kulima zaidi mihogo kwa sababu mahitaji yatakuwa makubwa, soko lipo linafikika… litakwenda kuchochea haja ya kuongeza kilimo katika maeneo hayo,” aliongeza.
Akiwa Pangani, pia Rais Samia alikabidhi boti 35 kwa wavuvi wa Tanga ambazo alisema zinakwenda kuwasaidia wavuvi hao kufika hadi karibu na bahari kuu ambako walikuwa wanashindwa kufika wanapotumia boti za awali.
“Nilikuwa naambiwa kila boti inabeba si chini ya tani tatu hadi tano za samaki, haya ni mavuno makubwa sana na nimeuliza zinakwenda umbali gani… nimeambiwa zinakwenda mpaka karibu na bahari kuu, zinakwenda kuvuna huko boti ambazo zile boti za awali hazikuwa zinafika, wavuvi wetu wanavuna mazao mengi ya baharini,” alibainisha kiongozi huyo wa nchi.
Aliongeza: “Suala la Soko la Kimataifa la samaki pale Kipumbwi hapa Pangani, soko hili nalo litaleta ajira na litaleta sura mpya Pangani… litakuza uchumi wa wana-Pangani kupitia uchumi wa buluu”.

Vilevile, akimjibu Mbunge wa Pangani, Juma Awesso kuhusu kuiunganisha Pangani na visiwa vya Unguja na Pemba, Rais Samia alisema tayari kupitia sekta binafsi kuna boto za Zanferries zinazofanya safari zake kati ya Tanga na Unguja na Pemba.
Hivyo alisema upo uwezekano wa kuongeza boti na kuongeza safari ili Bandari ya Tanga pia ihudumie na Pangani.
“Kwa sababu kweli kule Zanzibar wana mahitaji makubwa ya nazi, ni vyema kuangalia uwezekano wa kuongeza safari, kama boti zitatoka Pangani kwenda kule itakuwa ni biashara nzuri sana,” alisema Rais Samia.
Aliahidi kuwa Pangani inabadilika na itaendelea kubadilika kwani serikali inakuja na mikakati mbalimbali ikiwamo kuanzisha kilimo kikubwa cha miwa katika Bonde la Pangani na kujenga viwanda vya sukari ili kujitosheleza na uzalishaji wa sukari.



