Bil 1.8 kuunganisha Kata ya Mbingu, Namwawala

KILOMBERO, Morogoro: WAKALA Wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA umekamilisha ujenzi wa daraja la chuma la mto Lwipa (Mabey Bridge) lenye urefu wa mita 27 na matengenezo ya barabara ya Kisegese – Chiwachiwa – Lavena yenye urefu wa Km 15 kwa gharama za Sh bilioni 1.8.
Kukamilika kwa daraja hilo limewezesha kuunganisha Kata ya Mbingu na Namwawala katika Halmashauri ya Mlimba, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero Mhandisi Sadiki Kalumi amesema ujenzi wa daraja hilo lililojengwa na wataalam kutoka TARURA litarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.
“Daraja hili lina urefu wa mita 27 limegharimu shilingi milioni 900, lakini pamoja na daraja kuna matengenezo ya barabara ambayo itajengwa kwa kiwango cha changarawe pamoja na makalavati kwa gharama ya Sh milioni 900 kufanya jumla ya Sh bilioni 1.8”.Ameongeza kusema
Mhandisi Sadiki amesema hapo awali wananchi walikuwa wakitumia gogo kuvuka kabla ya kujengwa kwa daraja la mbao ambalo lilikuwa si la uhakika kabla ya TARURA kujenga daraja la chuma katika mto huo na kuchochea shughuli za kilimo katika maeneo hayo ya Chiwachiwa na Kisegese.



