Bil 10/- kuboresha miundombinu chuo cha Tengeru

SERIKALI imeendelea kufanya uwekezaji katika kuboresha miundombinu ya  Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) kilichopo Wilaya ya Meru kwa kufanya uwekezaji wa bilioni 10.3.

Akizungumza katika mahafali ya 14 ya chuo hicho, mkuu wa chuo, DkBakari George ameishukuru serikali  kwa jitihada inazofanya kuimarisha taaluma na sekta ya maendeleo ya jamii ambapo katika chuo hiko pekee fedha za maendeleo kiasi cha Sh bilioni 6.3 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.

Pia katika mwaka wa fedha inatarajia kupeleka bilioni 4.1 na kufanya uwekezaji wa zaidi ya bilioni 10.3. katika miundombinu ya ndani kwa kipindi cha miaka mitatu.

Advertisement

“Tunaishukuru serikali kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia taasisi hiyo fedha zaidi ya bilioni 10.3 katika kipindi cha miaka mitatu, fedha ambazo zimewekezwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya miundombinu ya chuo,” amesema Dk. George.

Katika mahafali hayo ya 14 kwa mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya Wanafunzi 1652 ambao wanawake 1,118 na wanaume 534 wamefuzu na kutunukiwa shahada za uzamili,shahada za kwanza,stashahada na astashahada katika chuo hicho.

Aidha Dk George amefafanua kuwa chuo kinaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la ghorofa tatu  ambalo lina jumla ya ofisi 44 , kumbi tano za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja na hadi  kukamilika kwake na mradi huo unatekelezwa na fedha kutoka Serikali Kuu  utatumia Sh bilioni  5.6.

Naye Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amewataka wahitimu kushughulika na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na mabadiliko tabia ya nchi pamoja na  na mmomonyoko wa maadili.

Ameongeza kuwa serikali imeweka mkazo katika uendeshaji na uiamrishaji wa sekta ya maendeleo ya jamii kama ambavyo jitihada kubwa zimefanyika na zinaendelea kuimarishwa kwa  huduma za jamii elimu,afya maji na barabara na kusema wizara itaendelea kuboresha miundombinu ya chuo hicho.