Bilionea wa Tanzania aipa heshima Afrika Mashariki

RIPOTI mpya ya Africa Wealth Report 2025 iliyochapishwa na kampuni ya ushauri wa uwekezaji ya kimataifa Henley & Partners kwa kushirikiana na New World Wealth, imeibua taswira mpya ya bara la Afrika kwenye ramani ya utajiri duniani, huku Tanzania iking’ara kama nchi pekee ya Afrika Mashariki yenye bilionea.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa Afrika ina jumla ya mabilionea 25, centi milionea 348 (wenye utajiri usiopungua dola milioni 100) na zaidi ya mamilionea 122,500. Hali hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya mwishoni mwa karne ya 20 ambapo mataifa mengi ya Afrika yalikuwa na mabilionea wachache na uchumi uliodorora.
Mataifa Kinara
Afrika Kusini inaongoza barani kwa kuwa na mabilionea wanane, ikifuatiwa na Misri (7), Morocco (4), Nigeria (3), huku Algeria, Seychelles na Tanzania zikiwa na bilionea mmoja mmoja. Kwa pamoja, mataifa hayo saba yanamiliki karibu asilimia 88 ya mabilionea wote barani Afrika.
Tanzania imeweka alama muhimu kwa kuingia kwenye orodha hiyo kama nchi pekee kutoka Afrika Mashariki, hatua inayoonyesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa uchumi. Kenya yaongoza kwa mamilionea, siyo mabilionea.
Hata hivyo, ripoti imebainisha kuwa Kenya haina bilionea, lakini imepanda chati kwa kuwa na mamilionea wengi zaidi ukilinganisha na majirani zake. Kwa sasa Kenya ina takribani mamilionea 6,800, na imeingia katika orodha ya nchi tano bora barani Afrika kwa idadi ya mamilionea, ikitanguliwa na Afrika Kusini (41,100), Misri (14,800), Morocco (7,500) na Nigeria (7,200).
Mtazamo wa Baadaye
Ripoti inatabiri kuwa idadi ya mamilionea Barani Afrika itaongezeka kwa asilimia 65 ndani ya muongo mmoja ujao, jambo linaloashiria fursa kubwa ya uwekezaji wa muda mrefu. Ukuaji huu unatarajiwa kufanikishwa na kasi ya uchumi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 3.7 mwaka 2025 na asilimia 4.1 mwaka 2026, kiwango kinachozidi ile ya Ulaya (0.7%) na Marekani (1.4%).
Nchi Zinazokua na Zilizodorora
Mauritius imeibuka kinara wa bara la Afrika kwa ukuaji wa watu wenye utajiri mkubwa (HNWI), ikirekodi ongezeko la asilimia 63 katika kipindi cha miaka 10, ikifuatiwa na Rwanda (48%) na Morocco (40%). Hata hivyo, baadhi ya nchi zimeporomoka kwa idadi ya mamilionea, zikiwemo Nigeria (-47%), Angola (-36%) na Algeria (-23%).
Kauli ya Wataalamu
Dominic Volek, Kiongozi wa Idara ya Wateja Binafsi wa Henley & Partners, amesema Afrika sasa imejitokeza kama mhimili mpya wa utajiri duniani. “Soko la uhamiaji wa uwekezaji linafanya kazi kwa pande mbili: Waafrika wanatafuta fursa zaidi kimataifa, huku wawekezaji wa nje wakitazama Afrika kama eneo salama na lenye fursa za uwekezaji wa muda mrefu,” amesema Volek. SOMA: Uwekezaji mkubwa sekta ya madini mapato yaongezeka