Bima ya Afya kwa Wote kutibu figo, moyo

Katika juhudi za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, Serikali kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote imeahidi kushughulikia changamoto zote zilizokuwepo kwenye mfumo wa sasa wa bima, ikiwemo kutokuwepo kwa huduma kwa baadhi ya magonjwa sugu.

Akizungumza leo Septemba 27, 2025 katika mjadala wa Cafetalk uliofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya afya.

“Ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwa Rais Dkt. Samia, Serikali itakuwa imekamilisha mchakato wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Mpango huu utashughulikia mapungufu yote yaliyopo kwenye vifurushi vya sasa vya bima ya afya,” amesema Hapi.

Ameeleza kuwa kupitia mpango huo mpya, matibabu ya magonjwa yote makubwa kama saratani, magonjwa ya moyo, figo na kisukari, ambayo awali yalikuwa nje ya huduma za bima, sasa yatagharamiwa kikamilifu na Serikali.

“Gharama zote za matibabu ya magonjwa haya makubwa zitabebwa na Serikali kupitia bima hii mpya, ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa huduma kwa sababu ya uwezo wa kifedha,” amesisitiza.

Mpango huu unatajwa kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa za haki, jumuishi na zenye kugusa maisha ya kila mwananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button