Dk Biteko: Uchaguzi 2025 si wa majaribio

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Doto Biteko, amesema uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 si wa majaribio, bali ni mchakato unaohusu maisha ya wananchi katika nyanja za elimu, afya, barabara, maji na ustawi wa familia.
Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe, wilayani Mbogwe mkoani Geita
Biteko aliwaomba wananchi waendelee kuiamini CCM kwa kuwa imeleta maendeleo makubwa yanayoonekana kwa macho.
“Watu wa Mbogwe asili yao ni watulivu na wakiahidi jambo wanalitekeleza. Hii si kwa bahati mbaya, bali kwa sababu mmeona maendeleo kwa macho yenu,” alisema.
Aliongeza,” Zamani mtu akisemekana anatoka Mbogwe ilikuwa ni jambo la kubezwa, lakini leo watu wanapita kifua mbele kwa sababu ya maendeleo yaliyofanikishwa na CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Biteko.
Alisema wananchi wanapaswa kuondoa mashaka kwa kuendelea kuiunga mkono CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kimejipambanua kwa vitendo kupitia utekelezaji wa Ilani yake.
“Uchaguzi huu ni wa kuamua mustakabali wa maisha yetu na mustakabali wa familia zetu. Kazi tuliyonayo ni moja tu, kujitokeza kwa wingi Oktoba 9 na kupiga kura. Ningetamani siku hiyo kuona misururu mirefu ya wapiga kura, maana kuna watu wanasubiri kasoro ndogo ili kuhoji,” alisisitiza.