Bodaboda Kigoma waonywa uhalifu

KIGOMA: Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Alli Ussi amewataka maofisa usafirishaji wa pikipiki za abiria maarufu kama ‘bodaboda’ kutotumia usafiri huo kuchochea vitendo vya uhalifu na badala yake pikipiki hizo ziwe sehemu ya kutoa ajira na kurahisisha usafiri.
Ussi amesema hayo wilayani Kasulu jana wakati mwenge wa uhuru ukianza mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu na kukabidhi mikopo ya Sh milioni 90 kwa kikundi cha bodaboda ‘Tushikamane’ kijiji cha Kalimungoma wilayani Kasulu ambacho kimenunua pikipiki 29 kupitia mkopo huo uliotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani.
Kiongozi huyo alisema kuwa tofauti na dhana inayojengwa kwamba waendesha bodaboda ni wahuni au wanafanya matendo ya kihuni ni vizuri kikundi hicho kuonyesha mfano kwa vitendo katika kuzitumia kutengeneza ajira lakini pia kuwa sehemu ya kuingiza kipato kwa bodaboda hao lakini chanzo cha mapato ya serikali kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali.

Sambamba na hilo kiongozi huyo ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha mikopo ya uwezeshaji kwa vikundi vya vijana, wanawake na makundi maalum inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani ni lazima na siyo hiari hivyo kila halmashauri lazima itekeleze maelekezo hayo ya serikali.
Mkuu wa Wilaya Kasulu, Isack Mwakisu akizungumza wakaati akipokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Kibondo, Agrey Magwaza alisema kuwa ukiwa wilayani humo mwenge huo wa uhuru utakimbizwa katika halmashauri mbili za wilaya hiyo kwa umbali wa kilometa 123 ikitembelea miradi 14 yenye thamani ya Sh bilioni 2.7.




