Bodi ya Chai, Japan wajadili thamani ya chai

BODI ya Chai Tanzania (TBT) imesema ujio wa ujumbe wa watu watano kutoka kampuni mbili kubwa za chai za Japan za Kawasaki Kiko na Nasa Corporation unatarajiwa kuleta mapinduzi ya viwanda vya teknolojia vitakavyosaidia kuongeza thamani ya zao hilo kimataifa.
Akizungumza Dar es Salaam leo kwenye mkutano na ujumbe huo uliojadili uzalishaji wa zao hilo na namna ya kuongeza thamani Kaimu Mkurugenzi wa TBT Beatrice Banzi amesema wanatarajia mapinduzi makubwa baadaye ya kiuwekezaji yatakayosaidia kuinuka kiuchumi.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Ofisa Balozi anayeratibu masuala ya uchumi wa Tanzania nchini Japan Edna Chuku imekuja baada ya bodi hiyo kutembelea Japan Julai mwaka huu kujifunza namna wanafanya katika uzalishaji. Ugeni huo utakuwepo nchini kwa siku tano ukitembelea mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya na Njombe.
“Tunachotarajia sisi ni mapinduzi ya viwanda tuna nguvu kazi lakini mitaji ya kuwalipa wale wafanyakazi wa viwanda itakuwa pungufu kidogo, tutakapotumia viwanda vya teknolojia itasaidia kupunguza gharama nyingine hapo baadaye.,”amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Balozi anayeratibu masuala ya uchumi katika ubalozi wa Tanzania nchini Japan Edna Chuku amesema ujio wa ujumbe huo ni katika jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kwenye kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Amesema wameona kwamba zao la chai linahitaji kuongezewa thamani kama yalivyo mazao mengine yanayofanya vizuri na wao wameliangazia katika kutafuta wawekezaji pamoja na masoko.
“Tunaenda kufanikiwa kwasababu wenzetu wa Japan wameonesha dhamira ya kufanikiwa katika sekta ya chai ikizingatiwa kule kwao hawana nguvu kazi na uzalishaji wao ni mdogo kutokana na jiografia yao kwa hiyo wanategemea kutafuta malighafi mbalimbali duniani Tanzania ikiwa miongoni,”amesema.

Mkurugenzi Mkuu wakala wa maendeleo ya wakulima wadogo wa Chai Tanzania Theophord Ndunguru amesema baada ya wao kujifunza kule Japan TBT imeanza mkakati wa kununua mashine kuongeza thamani ya zao hilo na kuipongeza bodi hiyo kwa ugeni huo utakaoleta manufaa.
Mwakilishi kutoka kampuni ya Nasa Corporation Gaelle Lagrouas amesema anaamini wanaweza kuisaidia Tanzania katika uzalishaji wa chai yenye thamani kupitia mashine ambazo wamekuwa wakizitengeneza.
Amesema hizo zinaweza kuwa msaada kwa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na mapato yataongezeka kwa kuuza bidhaa zao katika masoko ya kimataifa.




