Bomba la mafuta lapata ufadhili mradi ukifika 55%

MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umepata sehemu ya kwanza ya ufadhili wa nje.
Ufadhili kutoka kwa muungano wa taasisi za kifedha unaonesha imani katika ufanisi wa mradi huo na uwezo wake wa kuleta mageuzi katika sekta ya nishati ya Afrika Mashariki.
Washirika wa kifedha wanaounga mkono mradi huo ni pamoja na benki za kikanda kama African Export-Import Bank (Afreximbank), The Standard Bank of South Africa Limited, Stanbic Bank Uganda Limited, KCB Bank Uganda na The Islamic Corporation for the Development of the Private Sector (ICD).
Kukamilika sehemu ya kwanza ya ufadhili ni hatua muhimu kwa EACOP na wanahisa wake.
Wanahisa hao ni Total Energies (62%), Uganda National Oil Company Limited (UNOC 15%), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC 15%) na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC 8%).
Ujenzi wa bomba hili la urefu wa kilometa 1,443 unajumuisha kilometa 296 nchini Uganda na kilometa 1,147 nchini Tanzania.
Kufikia Machi mwaka huu maendeleo ya mradi yamefika asilimia 55 na zaidi ya raia 8,000 wa Uganda na Tanzania wameajiriwa katika mradi huo.

Mradi wa EACOP ukikamilika, bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha hadi mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku kutoka Kabaale, Wilaya ya Hoima nchini Uganda, hadi kwenye rasi ya Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.
Aidha, mradi huu umeunganishwa na gridi za kitaifa za umeme, ambazo zinategemea nishati ya maji, kupunguza athari za kaboni.
Mradi wa EACOP unawakilisha zaidi ya bomba la kusafirisha mafuta; ni alama ya ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa viwanda.

Kwa msaada wa taasisi kuu za kifedha na dhamira ya maendeleo endelevu, EACOP imejizatiti kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi Afrika Mashariki



