Bonde la Pangani mambo safi Mradi WAA

KILIMANJARO; BONDE la Pangani limechaguliwa rasmi kuwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Tathmini na Uhakiki wa Rasilimali za Maji (WAA) nchini, hatua muhimu katika kuboresha usimamizi wa maji na kuweka msingi wa matumizi bora ya rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Katika kutekeleza mradi hou, Bodi ya Maji Bonde la Pangani ilifanya warsha ya uthibitisho wa wadau wa WAA kwenye ofisi zake zilizopo Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro. Warsha hiyo ilikusudia kuhakikisha kuwa rasilimali za maji zinatunzwa, zinatumika kwa usawa, na zinakuwa na usimamizi endelevu.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule, alisema utekelezaji wa WAA utasaidia kupata takwimu sahihi kuhusu hali, matumizi, na mgawanyo wa rasilimali za maji, jambo litakalosaidia serikali na wadau kufanya maamuzi sahihi katika usimamizi wa maji.
Alisisitiza kuwa changamoto kubwa katika upatikanaji wa maji zinatokana na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi ya watu, na mahitaji ya maji kwa shughuli za kiuchumi.

Alihimiza wananchi kutumia maji kwa uangalifu, kulinda vyanzo vya maji, na kufuata sheria na taratibu zinazowekwa na serikali.
“Matumizi sahihi ya maji na ufuataji wa sheria ni wajibu wa kila mwananchi ili kulinda rasilimali hii muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisisitiza Segule.
Bodi ya Maji Bonde la Pangani imewahimiza wananchi kushirikiana na taasisi husika katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, kuripoti matumizi yasiyo halali ya maji, na kuchangia juhudi za utunzaji wa mazingira.

Warsha hii imewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Maji, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi, asasi za kiraia, wataalamu wa maji, pamoja na jumuiya za watumia maji, kwa lengo la kupitia na kuthibitisha taarifa ya tathmini ya rasilimali za maji ya Bonde la Pangani.



