BRELA kutatua changamoto za usajili wafanyabiashara Kariakoo

DAR ES SALAAM: Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeanzisha kliniki ya biashara kwa wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam ili kutatua changamoto mbalimbali za usajili na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Kupitia kliniki hiyo, BRELA inalenga kuwahudumia wafanyabiashara kwa kuwawezesha kurasimisha biashara zao kwa kusajili majina ya biashara, kampuni, alama za biashara, pamoja na kupata leseni za biashara.

Akizungumza katika uzinduzi wa kliniki hiyo, mmoja wa maafisa wa BRELA alisema kuwa huduma hiyo imelenga kuongeza mwamko wa wafanyabiashara kurasimisha shughuli zao ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kisheria.

Aidha, BRELA imepanga kufanya ukaguzi wa maduka kwa mtazamo wa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na Leseni ya Biashara Kundi A, hasa kwa wale wanaojihusisha na biashara zenye mwelekeo wa kimataifa.

Kampeni hii inalenga kuongeza uelewa wa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuendesha biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali, huku ikihamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha mchakato wa usajili.

Wafanyabiashara wa Kariakoo wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo na kujipatia elimu juu ya namna bora ya kusimamia na kukuza biashara zao kwa njia rasmi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button