BRELA wapongezwa uboreshaji mifumo kidijitali

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza Taasisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa hatua kubwa ilizochukua katika kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya kidijitali, ikiwemo utoaji wa leseni na usajili wa biashara kwa kuwa yamesaidia kuongeza kasi ya usajili wa biashara na utoaji wa leseni nchini.
Waziri Kapinga ametoa pongezi hizo leo, Novemba 27, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo kwa lengo la kujionea jinsi inavyotekeleza majukumu yake, ambapo amebainisha kuwa moja ya mafanikio makubwa ya BRELA ni kuongeza vyanzo vyake vya mapato, na kufanikiwa kuchangia takribani Sh bilioni 82 kama gawio kwa Serikali.
Aidha, Waziri Kapinga amesema kuwa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya mwaka 2050 ya kuhakikisha vijana wanapata ajira milioni nane na kuanzisha mfuko maalumu wa vijana, BRELA inapaswa kuongeza ubunifu na ufanisi ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa trilioni kadhaa.
“Tukiendelea kusajili viwanda vingi zaidi na biashara nyingi zaidi, tutaongeza ajira na kuleta maendeleo ya uchumi kwa taifa letu. Tunawapongeza sana BRELA, na tumesisitiza umuhimu wa ufanisi, weledi, maadili na kupenda kazi ili kuleta matokeo kwa Watanzania,” amesema Kapinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema taasisi yake imepokea ushauri wa Waziri Kapinga na itaendelea kufanya maboresho zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya huduma za BRELA zinategemea mifumo ya kidijitali, na kwamba wataendelea kuboresha miundombinu ya utendaji kazi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wake.
Nyaisa amefafanua kuwa BRELA imeunganishwa na taasisi mbalimbali kama NIDA, TRA na baadhi ya mabenki, hatua inayorahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu na kupunguza mzunguko wa kupata huduma. Aliongeza kuwa kipaumbele cha BRELA ni kutoa huduma bora kwa taasisi binafsi ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja.
Kwa sasa, BRELA inaendelea na kampeni za uelimishaji kwa umma kuhusu huduma zake, pamoja na kufanya ukaguzi wa biashara na viwanda ili kuongeza ufanisi na kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa biashara nchini.



