CAF, UEFA shirika watoa elimu saratani shingo ya kizazi

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ulaya (UEFA), na Shirika la Gavi wameungana kupitia mashindano ya GIFT (Girls Integrated Football Tournament) kutoa elimu kuhusu chanjo ya HPV kwa lengo la kuzuia saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana.

Akizungumza katika warsha maalumu iliyofanyika leo katika Dar es Salaam,  Mkuu wa Soka la Wanawake wa CAF, Meskerem Tadesse Goshime, amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha afya za wachezaji zinaimarika.

“Wasichana 150 kutoka timu saba za ukanda wa Afrika Mashariki wanashiriki kwenye programu hii. Ni muhimu kwa sababu hatua za kinga dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi zichukuliwe wakiwa bado vijana. Hii ni sehemu ya sera yetu ya kutumia mpira wa miguu kama chombo cha maendeleo na elimu,” amesema Goshime.

Naye mtangazaji wa michezo na mtendaji wa soka kutoka Uingereza, Eniola Aluko, amesisitiza umuhimu wa chanjo ya HPV kama njia ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi. Ameeleza kuwa elimu inayotolewa kwa wasichana hao inalenga kubadilisha mitazamo potofu kuhusu masuala ya afya ya uzazi na kuongeza ufahamu wa jamii kwa ujumla.

Elizabeth Makora, mshiriki kutoka timu ya Kenya, alisema warsha hiyo imempa uelewa zaidi kuhusu HPV na njia za kujikinga. Aliongeza kuwa ataendelea kuwa balozi wa kuelimisha jamii yake kuhusu umuhimu wa chanjo ili kufanikisha ndoto za wasichana wengi bila vikwazo vya kiafya.

Mashindano ya GIFT yanayowalenga wachezaji wa chini ya miaka 17 ni ya kipekee, yakilenga si tu kukuza vipaji vya mpira wa miguu bali pia kuimarisha afya na elimu ya kijamii kwa kutumia mpira kama daraja la mabadiliko chanya

Habari Zifananazo

Back to top button