CCM: Huwezi kumkwepa Samia
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kama Watanzania wanapiga kura za uchaguzi wa rais kwa kuzingatia matokeo, hakuna namna ya kutomchagua mgombea kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan.
Mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema hayo wakati wa mkutano wa kampeni Mombo, Korogwe Vijijini.
Dk Nchimbi amesema Samia hana deni na Watanzania kwa kuwa amefanikisha mageuzi katika sekta za elimu, afya, kilimo, uvuvi, ufugaji, umeme na biashara.

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kama Watanzania wanachagua kwa kuangalia matokeo, hakuna namna ya kumkwepa Samia,” amesema Dk Nchimbi na akasema serikali ya CCM itaongeza kasi ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo.
Uteuzi wagombea CCM
Dk Nchimbi amesema demokrasia ndani ya chama huzingatia misingi ya nidhamu na uongozi wa kubadilishana kijiti.
Amesema hayo katika mkutano wa kampeni Soni wilayani Lushoto katika Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga.
Dk Nchimbi amesema kila chama cha siasa kina utaratibu wa kuteua wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais.
SOMA: Sumaye amsifu Dk Samia
“Mtu akiachwa leo si maana yake ataachwa kesho. Unaweza leo ukaachwa kwa nafasi moja lakini ukapewa nafasi kubwa zaidi baadaye. Mwaka 2015 mimi niligombea uspika, lakini sikuteuliwa. Baada ya miaka 10, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM imeniteua kuwa mgombea mwenza wa urais. Uongozi ni kupeana kijiti,” alisema.
Dk Nchimbi amesisitiza umuhimu wa nidhamu katika demokrasia akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwamba demokrasia bila nidhamu ni fujo.
“Lazima tuendeshe demokrasia lakini inayoambatana na nidhamu,” amesema.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesifu wananchi wa Lushoto kwa kujiletea maendeleo kupitia shughuli za kilimo, biashara ndogondogo, viwanda vidogo, uvuvi, uchimbaji madini na mazao ya misitu.
“Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Lushoto wanategemea kilimo, mboga, matunda, viungo na mazao mengine yanapatikana hapa. Hongereni sana, mnatupa heshima kubwa,” amesema.

Pia, Dk Nchimbi alimshirikisha Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba kupitia mawasiliano ya simu ambaye aliwaomba wananchi wa Jimbo la Bumbuli kumchagua Samia, mgombea ubunge wa jimbo hilo Ramadhani Singano na madiwani wote wa CCM.
“Naamini kwa moyo wangu wote kwamba CCM itashinda majimbo yote ya Mkoa wa Tanga. Nilitamani sana kuwepo nanyi leo, ila changamoto za afya zimeniweka pembeni. Nawataka msimuangushe Rais Samia, wabunge na madiwani wote wa CCM katika Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025,” amesema Makamba.
Dk Nchimbi ametaja baadhi ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa Korogwe Vijijini kuwa ni pamoja na kuboresha hospitali ya wilaya kwa kuongeza majengo, huduma na vifaatiba, kujenga vituo vya afya viwili vipya, kuongeza zahanati sita, shule tatu za sekondari, shule tano za msingi, maabara 15, mabweni 21 na nyumba mpya 61 za walimu.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, amesema skimu za umwagiliaji zitaongezwa pamoja na ruzuku ya pembejeo na viuatilifu.
Aidha, kiwango cha upatikanaji maji safi na salama kitapanda kutoka asilimia 75 hadi kufikia asilimia 90 ndani ya miaka mitano ijayo, sambamba na uboreshaji wa barabara kwa kiwango cha changarawe na lami.
Mgombea ubunge Korogwe Vijijini kupitia CCM, Timotheo Mnzava amesema utekelezaji wa ilani ya chama hicho utaendelea kwa kasi kubwa zaidi.
“Hatuna deni na serikali ya CCM. Tumejipanga kupiga kura nyingi za heshima kwa wagombea wetu. Tunaomba Mombo ipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji, ijengwe stendi ya mabasi ya kisasa na soko la kisasa,” amesema Mnzava.
Mgombea ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso amesema serikali imetenga Sh bilioni 900 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji Mombo.



