CCM Iringa yapokea viongozi wa Chaumma Iringa na Njombe

IRINGA: Wimbi la hamasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni za ubunge jimbo la Iringa Mjini limeendelea kushika kasi baada ya viongozi wa chama cha Chaumma mikoa ya Iringa na Njombe, wakiongozwa na wenyeviti wao wa mikoa na makatibu, kutangaza kujiunga rasmi na CCM katika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliofurika katika mkutano huo uliofanyika kata ya Kihesa, Yasin alisema CCM inaendelea kuaminiwa kutokana na utekelezaji wa vitendo wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025, ambao umeleta matokeo halisi kwa wananchi.

“Ahadi za mwaka 2020 hadi 2025 zimetekelezwa kwa kiwango kikubwa. Wana Iringa tunakuja kifua mbele, msiwe na mashaka juu ya utekelezaji wa ahadi. Desturi yetu ni moja – tukitoa ahadi, tunatekeleza,” alisema Yasin huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya 2025-2030, miradi mikubwa ya maendeleo katika jimbo la Iringa itatekelezwa kwa kasi chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

“Katika sekta ya afya, tumeahidi kujenga zahanati mpya mbili na vituo vitatu vya afya, kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Frelimo,” alisema Yasin.

Akiendelea kutaja ahadi za CCM kwa jimbo hilo, Yasin aligusia sekta ya elimu akisema; “Katika elimu, tutajenga vyumba 294 vya madarasa katika shule za msingi na sekondari, maabara 40, mabweni manane, mabwalo saba ya chakula, matundu 1,000 ya choo, na tutakarabati shule kongwe mbili za sekondari. Hii ni kazi ya CCM kwa vitendo,” alifafanua.

Aliongeza kuwa sekta ya biashara na uwezeshaji wananchi kiuchumi pia imepewa kipaumbele.

“Tutajenga soko kubwa la kisasa la Machinga Complex pale Stendi Kuu ya zamani, tutakamilisha stendi ya mabasi ya Igumbilo, tutakarabati masoko saba ya manispaa na machinjio ya kisasa Ngelewala. Vilevile, tutajenga ofisi 40 za mitaa na tutaboresha utoaji wa mikopo kwa vikundi zaidi ya 500 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” alisema.
Yasin alisema ahadi hizo zinaonesha dhamira ya CCM ya kuimarisha uchumi wa wananchi na kuboresha huduma za kijamii bila upendeleo.

“Msisikilize porojo juu ya ukweli wa utekelezaji wa ahadi zetu. Dk Samia amekuwa mfano wa uongozi wa vitendo,” alisema.

Miongoni mwa waliojiunga na CCM ni Mwenyekiti wa Chaumma Mkoa wa Iringa, Diana Benedikto, ambaye pia ni mjumbe wa sekretarieti ya taifa ya chama hicho, pamoja na Katibu wa Mkoa wa Iringa, Ibrahim Idd. Kutoka Mkoa wa Njombe waliojiunga ni Mwenyekiti Makuke Mjinja na Katibu wake, Diana Kivina.

Ibrahim Idd alisema uamuzi wake wa kurejea CCM umetokana na ukweli na uadilifu wa chama hicho.

Kwa upande wake, Diana Benedikto alisema;
“Nimeamua mwenyewe kurudi CCM kwa sababu kule Chaumma hakuna jipya. Kule tunaambiwa tunakula ubwabwa, lakini huku kuna amani na maendeleo. Msifanye mchezo na kitu kinachoitwa amani.”

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya, alisema kampeni za mwaka huu zimefanyika kwa amani na kwa ufanisi mkubwa.

“Hakuna nyumba ambayo hatujapita, tumekutana na taasisi, viongozi wa dini, mafundi gereji na vilabuni. Tulinadi Ilani ya CCM, tukatoa elimu ya upigaji kura, na wananchi wamempokea vyema mgombea wetu,” alisema Rubeya.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo awamu iliyopita, Jesca Msambatavangu, aliwahimiza wananchi na vyama vyote kuweka mbele maslahi ya taifa.

Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali pamoja na taasisi zingine za kifedha zitaboresha upatikanaji wa mikopo na kukuza ujasiriamali kwa vitendo.

“Tutahakikisha mikopo inatolewa kwa wakati. Tutatahakisha mnakopeshwa vifaa vya kazi, si fedha tu, ili tuwezeshe wajasiriamali kukua kutoka hatua ya chini hadi juu,” alisema.

Katika sekta ya michezo, Ngajilo aliahidi kuhakikisha Iringa inapata timu atakayoipambania hadi Ligi Kuu kupitia mashindano ya kata.

“Nataka kuona Kkla kata ina timu, kisha tuunde timu moja ya manispaa tutakayoibeba hadi Ligi Kuu. Iringa lazima irudi katika ramani ya michezo,” alisema kwa kujiamini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button