CCM yaahidi bandari ya kisasa Bagamoyo

PWANI: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa endapo kitapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu ujao, kitaendeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari ya kisasa katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
 
Akizungumza leo, Septemba 28, 2025, wakati wa kampeni zake kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema bandari hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa fursa za kiuchumi kwa Watanzania wote.
 
Dk. Samia amesema bandari hiyo ya Bagamoyo itakuwa na gati za kisasa zitakazokuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi kuliko zile zinazopokelewa sasa katika Bandari ya Dar es Salaam, ili kuongeza uwezo wa nchi katika kushughulikia biashara ya kimataifa na kukuza uchumi wa taifa.
 
Ameongeza kuwa bandari hiyo itaunganishwa na Reli ya Kisasa (SGR) kupitia kipande cha kilomita 100 kutoka Bandari Kavu ya Kwala hadi bandari hiyo mpya, jambo litakalorahisisha usafirishaji wa mizigo kwa kutumia miundombinu ya kisasa.

Mbali na hilo, Dk. Samia amesema kutajengwa eneo maalumu la kiuchumi lenye ukubwa wa hekta 9,800 karibu na bandari hiyo, ambalo litalenga kuchochea uzalishaji na kuvutia wawekezaji wa viwanda ndani na nje ya nchi.

Aidha, amebainisha kuwa upembuzi yakinifu wa mradi huo tayari umekamilika, na utekelezaji wake utafanyika kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na sekta binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button