CCM yaja na mikakati ya mageuzi Dar

DAR-ES-SALAAM : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuwaletea wakazi wa Dar es Salaam mapinduzi makubwa ya kimaendeleo katika sekta za miundombinu, ardhi, usafi rishaji, uchumi, ajira na biashara, ikiwemo kujenga stendi ya kisasa na kukamilisha Mradi wa Mwendokasi Awamu ya Pili Mbagala ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030.
Kimepanga pia kuhakikisha kinakamilisha changamoto ya vivuko katika maeneo yote yenye uhitaji na kuhamasisha wananchi wenye ardhi kubwa kuziendeleza kuondokana na mapori yanayoficha vibaka.
Mgombea mwenza wa urais, Dk Emmanuel Nchimbi alitoa ahadi hizo akihutubia wananchi katika Viwanja vya Mjimwema Kigamboni na Maturubai Polisi Mbagala, Dar es Salaam jana. Akiwa Mbagala, Dk Nchimbi alisema mradi wa barabara za mwendokasi umekamilika kujengwa na tayari mabasi 155 yamewasili nchini, yakisubiri kukamilishwa kwa taratibu za kiutendaji ili yaanze kutoa huduma.
“Nia ya CCM katika miaka mitano ijayo ni kuondoa changamoto ya foleni kwa kupanua barabara nne hadi sita, kujenga daraja la juu la Uhasibu Chang’ombe na kuendelea na ujenzi wa barabara za ndani, pembezoni na mbadala,” alisema. SOMA: JK: Samia atapata kura za kihistoria Pwani
Alisema CCM imepanga kujenga stendi mpya ya kisasa ya mabasi Mbagala yenye vizimba na maduka, itakayokuwa kitovu cha usafiri wa Kusini mwa Tanzania na pia Bandari Kavu ya Kurasini itajengwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za bidhaa na kuongeza ushindani wa kiuchumi.
Akizungumzia uchumi, Dk Nchimbi alisema biashara zimeimarika katika miaka minne iliyopita kutokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa rafiki wa wafanyabiashara badala ya kuwa adui.
Akiwa Kigamboni, Dk Nchimbi alisema miongoni mwa miradi mikubwa ya barabara itakayotekelezwa ni kukamilisha kwa kiwango cha lami Barabara ya Kibada– Mwasonga–Kimbiji, Barabara ya Kibada–Stendi na Barabara ya Mjimwema–Pembamnazi na Marasinge–Tungi. Aliahidi pia uboreshaji wa barabara ndogondogo za mitaa kwa kiwango cha lami ikiwemo Full Shangwe–Kibada na Gezaulole–Mivumoni.

Alisema upanuzi wa maegesho kwenye kivuko cha Magogoni na Kigamboni ili kupunguza foleni na matengenezo ya haraka ya vivuko vya MV Magogoni na MV Kigamboni kupunguza gharama kwa wananchi.
Katika sekta ya afya, alisema CCM imepanga kuiboresha zaidi Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni ili iweze kutoa huduma za kibingwa, kujenga vituo vya afya sita vipya na kuongeza wigo wa huduma za afya karibu na wananchi.
Kwenye elimu, alisema shule za sekondari nne mpya zitajengwa Kigamboni, kati ya hizo tatu zitakuwa za kufundisha kwa kiwango cha mchepuo wa Kiingereza ili kuwapa fursa watoto wa familia za kipato cha kawaida kusoma katika shule hizo bila gharama kubwa.
Kuhusu maji, alisema ndani ya miaka mitatu ijayo, CCM itakamilisha mradi wa visima saba unaoendelea, kuanzisha mradi mpya wa visima virefu tisa, kujenga matangi makubwa ya kuhifadhi maji na kupanua mtandao wa usambazaji maji katika maeneo ya Pembamnazi, Kimbiji, Kisarawe II na Vijibweni.
Kuhusu ardhi na makazi nayo imepewa kipaumbele kwa kusimamia upimaji wa viwanja, upangaji wa miji na kuhamasisha wamiliki wa viwanja kuviendeleza ili kuondoa mapori ambayo yamekuwa kikwazo cha maendeleo na vimekuwa maficho ya wahalifu.
Alisema CCM imepanga kuanzisha viwanda vya kusindika samaki, mazao na juisi Kigamboni ili kuongeza ajira kwa vijana na kupandisha thamani ya mazao ya wakulima. Alieleza kuwa Kigamboni imepangwa kuboreshwa kuwa kitovu cha utalii kutokana na fukwe zake za kipekee ambazo zitavutia wageni wa ndani na nje ya nchi. Kuhusu ajira, Dk Nchimbi alisema CCM imedhamiria kutengeneza ajira milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi.



