CCM yakosa upinzani majimbo saba Geita

GEITA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita kimeweka wazi kuwa wagombea ubunge wa chama hicho kwenye majimbo saba ya uchaguzi kati ya tisa ya mkoa mzima wamekosa upinzani kutoka vyama vya upinzani.
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Nicolous Kasendamila ametoa taarifa hiyo katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za ubunge jimboni humo zilizofanyika kwenye viwanja vya CCM-Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro.
Kasendamila amesema hali hiyo inaashiria kuwa CCM ina uhakika wa kupita kwa asilimia kubwa kwenye majimbo saba huku majimbo mawili ya uchaguzi ndio wagombea ubunge wa vyama vya upinzani wamejitokeza.
“Kimsimgi hatuwatazami kama wapinzani, tunawaita vyama rafiki kwa sababu wanakwenda kusindikiza harusi wamejiandaa kujivika na ushungi, lakini bwana harusi atakayeingia kwenye chumba cha bibi harusi ni CCM.
“Tunakwenda kuyabeba majimbo yote tisa, kwa sababu siku ya Oktoba 29, 2025 watanzania wanakwenda kutiki kwa si kwingine bali ni kwa wagombea wa CCM”, amesema.
Kasendamila amewasisitiza wananchi wote mkoani Geita kujitokeza kwa uwingi kupiga kura kwani mbali na kuwa majimbo saba yamekosa upinzani bado wananchi wana mamlaka ya kuwapitisha au kuwakataa wagombea.
Kwa mjibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) majimbo tisa ya uchaguzi mkoani Geita ni Geita mjini, Jimbo la Geita, Nyang’hwale, Mbogwe, Busanda, Katoro, Bukombe, Chato Kusini na Chato Kasikazini.
Mpaka kuanza kwa mchakato wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 majimbo ambayo chama tawala cha CCM kimepata upinzani mkoani Geita ni jimbo la Mbogwe pamoja na Katoro.



