CCM yawapoza wahanga wa moto Iringa

“Tumeumia pamoja nanyi. Niwahakikishie—hatuwezi kuwageuzia mgongo. Tunasubiri tathmini na tutasaidia hapa na pale mrejee katika shughuli zenu. Na kama wahusika wa soko hili wakihitaji msaada wa kuboresha miundombinu, tutashiriki bila kusita.”

Ni kauli ya kusisimua iliyojaa utu na mshikamano kutoka kwa Salim Asas, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alipozungumza mbele ya mamia ya wananchi waliokusanyika katika Soko la Mashine Tatu lililoungua mjini Iringa.

Asas alikiri kwa masikitiko makubwa kwamba janga la moto lililoteketeza zaidi ya biashara 500 limeacha maumivu makubwa kwa wafanyabiashara wengi wa kipato cha chini, hasa wale waliokuwa wamechukua mikopo ya kujikimu kimaisha.

Kwa sauti ya faraja, Asas aliwahakikishia wahanga kuwa CCM iko nao bega kwa bega, na itahakikisha misaada, michango, na jitihada za kuwainua zinapangwa kwa utaratibu mzuri.

“Kama chama, tunawajali sana. Tutaendelea kuwa karibu nanyi hadi muingie tena sokoni ujasiri,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta alieleza kuwa eneo hilo linalomilikiwa na Bakwata tayari limeanza kupangiwa mipango ya marekebisho kwa kushirikiana na viongozi wa soko na serikali.

“Kwa tathmini yetu ya awali, vizimba vya ndani 450 vimeteketea kabisa, na biashara nyingine 85 za nje zimeathirika. Kwa jumla, biashara 535 zimeguswa na janga hili,” alisema Sitta.

Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa tayari wamekubaliana na Bakwata kuandaa mpango kazi maalum wa kuwarejesha wafanyabiashara sokoni.

Alisema hadi sasa, maeneo saba mbadala yameandaliwa kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga kwa muda.

“Waliochukua mikopo, wajiorodheshe haraka. Tupo tayari kuwaunganisha na taasisi zao na kuwaomba wasiwabane kwa sasa. Hatutaki mtu ajifungie nyumbani kwa sababu ya deni,” alisisitiza.

Katika juhudi za muda mrefu za kutatua changamoto ya maeneo ya biashara Iringa, Salim Asas alitangaza kuwa CCM kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wanapendekeza kujengwa kwa Machinga Complex kubwa katika eneo la stendi ya zamani.

“Manispaa imekubali na michoro ipo mbioni kukamilika. Itakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya machinga 1,000 pamoja na fremu pembeni. Hii ni fursa ya kujenga upya kwa ubora na usalama zaidi,” alisema Asas.

Mmoja wa wafanyabiashara waliopoteza mali zote, Jafari Maulid, alisimulia kwa uchungu jinsi alivyojionea mali zake zikiteketea mbele ya macho yake:

“Uhai wetu ni shughuli zetu. Soko hili lilikuwa namba moja kwangu. Nilifanikiwa kuokoa mawe tu ya mzani. Tunaomba serikali ituangazie—imeshakuwa kama kifungo cha damu.”
Kauli hiyo ilimfanya Asas kusisitiza kuwa misaada ya mitaji na michango ya kifedha itapangwa kwa makini na kuhusisha wahusika halali tu ili kuzuia ujanja ujanja wa baadhi ya watu wanaojaribu kujipenyeza.

Katika hatua ya kufunga mkutano huo wa faraja, Asas alituma ujumbe wa matumaini:
“Moto umechoma mali zenu, lakini haujaweza kuchoma ndoto zenu. Tutasimama nanyi, tutajenga nanyi, na tutainua maisha yenu upya. Amani tuliyonayo ni mtaji mkubwa kuliko yote—tuilinde.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button