CCM yaweka ukomo ubunge, udiwani Viti Maalumu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka ukomo wa ubunge na udiwani wa Viti Maalumu.

Taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Oganaizesheni, Issa Haji Ussi imeeleza kuwa uamuzi huo umefanywa na kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Dodoma kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Ussi alieleza kuwa CCM imeweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kwa nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani wa viti maalumu wanawake.

“Ukomo huo utaanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030,” alieleza.

Ussi alieleza kuwa kura za maoni kwa waombaji wa nafasi za ubunge/ uwakilishi wa viti maalumu wanawake kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi zitapigwa na wajumbe wa mikutano mikuu maalumu ya taifa.

“Mikutano mikuu ya Taifa ya UVCCM/Wazazi itakuwa na wajumbe wanawake tu,” ilieleza taarifa hiyo.

Ussi aliwataja wajumbe hao ni wajumbe wote wanawake wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa UVCCM/Wazazi, wajumbe wote wanawake wa Kamati za Utekelezaji za UVCCM/Wazazi za mikoa na wajumbe wote wanawake wa Kamati za Utekelezaji za wilaya UVCCM /Wazazi.

Akieleza kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, alisema Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imeridhia mapendekezo ya marekebisho ya kanuni hizo.

Alitaja maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi wa majimbo na udiwani wa kata/wadi na mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani wa viti maalumu wanawake.

Taarifa ilitaja eneo lingine lililofanyiwa marekebisho ni upanuzi wa wigo wa idadi ya wajumbe wa vikao vya chama na jumuiya zake watakaopiga kura za maoni.

“Lengo la hatua hii ni kuimarisha misingi ya demokrasia, uwazi na kupanua uwakilishi wa wanachama wa CCM katika kuwapata wagombea wa nafasi za uongozi katika chaguzi za vyombo vya dola,” alieleza Ussi.

Vilevile alisema kuwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imepitisha Kaulimbiu rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 isemayo,

‘Kazi na utu, tunasonga mbele’. Hivi karibuni, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Sophia Simba alisema viti maalumu ni vya kuwawezesha wanawake kwenda kugombea majimboni hivyo waliokaa kwa muda mrefu katika nafasi hizo wawaachie vijana.

Simba alisema UWT walishaweka ukomo wa ubunge wa viti maalumu miaka 10 lakini utekelezaji ukawa mgumu.

“Kama umekaa bungeni mpaka miaka 20 kwenye viti maalumu bado unashindwa kuingia kwenye jimbo, basi
huwezesheki, umeshindwa kujiwezesha, kukataa kuondoka ni kama choyo tu,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button