Chalamila akerwa uchafu soko la Feri
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema atalifunga kwa muda Soko la Kimataifa la Samaki Feri iwapo hali ya usafi haitaridhisha sokoni hapo hadi kufikia Januari 23, mwaka huu.
Alisema hayo jana sokoni hapo wakati wa usafi ulioanzia eneo la Kamata hadi sokoni hapo.
Chalamila alisema kuwa usafi unafanyika sokoni hapo lakini hali ya usafi bado hairidhishi hali inayosababisha kuwa na harufu.
“Mkuu wa wilaya nafahamu jinsi mnavyojitahidi kufanya kazi na mnafanya kazi nzuri na ndiyo maana hata uchafu si kama ilivyokuwa zamani wanaosimamia wanajitahidi lakini juhudi za usafi ziongezeke,’’ alisema.
Alisema kuwa Januari 27 hadi 28 taifa linatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika hivyo eneo hilo na mengine yanatakiwa kuwa safi muda wote.
Alisema kama watashindwa kufanya usafi, ataviagiza vikosi vya usalama kufanya usafi eneo hilo na kulilinda hadi mkutano huo utakapokwisha na wafanyabiashara watakapokuwa tayari kufanya usafi katika soko hilo.
Vilevile aliutaka uongozi wa soko hilo kufunga mifumo maalumu itakayowezesha wauzaji kuuza na kutoa risiti pamoja na kuziba mianya ya watu kukwepa kulipa kodi sokoni hapo ili kuongeza mapato ambayo yanatumika katika kutekeleza miradi mbalimbali.
Pia, Chalamila aliagiza kuharakishwa kwa mchakato wa kumpata mwekezaji atakayehudumia dampo la Pugu ili kupunguza gharama ambazo Halmashauri ya Jiji inatumia katika kununua vipuli na mafuta katika kuhudumia dampo hilo.
“Jumatatu asubuhi (kesho) nitatembelea dampo la Pugu ili kuangalia hii foleni iliyopo mjini na kule zinakopelekwa hali ipoje, mkurugenzi hii hali ya kununua mafuta na vipuli kila mara na kuleta hasara kubwa katika jiji tunataka tuikomeshe ili dampo la Pugu lipate mwekezaji mkubwa atakayezalisha ajira,” alisema.
Aidha, Chalamila alisema kuwa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utakapoanza barabara ya stesheni hadi feri itazuiliwa kwa baadhi ya vyombo vya moto ili kupunguza foleni kwa wageni watakaokuja. Aliagiza taa za barabarani kuwashwa wakati wa usiku kwa ajili ya kuongeza usalama.
Akizungumza kwa niaba ya wavuvi na wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri, Samwel Bernard alimuomba mkuu wa mkoa kufunga pampu itakayokuwa inatoa maji baharini hadi sokoni hapo kwa ajili ya matumizi ya usafi.



