Chalamila azindua Premier Clinic Muhimbili

DAR-ES-SALAAM : MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amezindua kliniki maalum ya Premier Clinic katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzira, yenye lengo la kutoa huduma binafsi na za kiwango cha juu kwa viongozi, watu mashuhuri na wenye uwezo wa kifedha wanaohitaji faragha zaidi katika matibabu yao.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Chalamila alisema sekta ya afya nchini imepiga hatua kubwa, hasa katika eneo la utalii tiba, na Tanzania imeanza kujipatia sifa kimataifa kwa kutoa huduma bora, ikiwemo upandikizaji wa figo na matibabu mengine kwa wagonjwa kutoka Malawi na Uganda.
“Afya ni eneo nyeti linalojitegemea. Hatuwezi kuchanganya afya na siasa. Kila mmoja anapaswa kupata huduma kulingana na uwezo wake, bila kupoteza utu wala heshima,” alisema. SOMA: Mlongazila kupandikiza meno bandia
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Delila Kimambo, alisema uzinduzi wa Premier Clinic ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 120 ya Muhimbili na miaka 25 tangu hospitali hiyo kutangazwa kuwa ya Taifa.
Naye Naibu Mkurugenzi, Dk. Julieth Magandi, alisisitiza kuwa huduma hiyo mpya itaongeza hadhi ya Tanzania katika ramani ya utalii tiba barani Afrika. Kutoka Wizara ya Afya, Dk. Asha Maita alieleza kuwa Tanzania inalenga kuingia katika orodha ya nchi tano bora Afrika katika huduma za utalii tiba, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa miradi ya afya.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, aliipongeza Hospitali ya Mloganzira kwa huduma bora wanazotoa na kusisitiza dhamira ya serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya.