Chaumma kuteua wagombea urais leo

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) leo kinateua wagombea urais wa Tanzania na Zanzibar.
Chaumma itateua wagombea hao katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho ambao pia utateua mgombea mwenza wa urais wa Tanzania na mgombea mwenza wa urais wa Zanzibar.
Pia, katika mkutano huo chama hicho kinatarajia kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano na Taarifa kwa Umma, John Mrema imeeleza mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Mrema alieleza ilani ya chama hicho inatokana na sauti ya wananchi na mahitaji ya taifa kwa sasa.
Alieleza kuwa mchakato wa vikao vya kuwapata wagombea wa urais vilianza Agosti 4 hadi 5, mwaka huu kwa vikao vya sekretarieti ya kitaifa ya maandalizi ya vikao vya ngazi ya juu.
Mrema alieleza jana chama hicho kilifanya mkutano wa Kamati Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu ya Taifa kupokea, kujadili na kupitisha ajenda za Mkutano Mkuu wa chama taifa.
Hivi karibuni Chaumma ilikaribisha wenye nia ya kugombea urais wa Tanzania na urais wa Zanzibar kuanzia Julai 29 hadi Agosti 4, mwaka huu.
Chama hicho kiliwataka wenye nia ya kugombea wawasilishe barua kwa Katibu Mkuu kuomba kuwania nafasi hizo.
Pia, Chaumma ilitangaza kuwa ukomo wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo, ubunge viti maalumu, uwakilishi, uwakilishi viti maalumu na udiwani viti maalumu ni kesho.
Agosti 16 hadi 17, mwaka huu kamati za utendaji za mikoa zitaketi kuchakata na kuandaa taarifa za wagombea na kutoa mapendekezo kwa Sekretarieti ya Taifa.
Kadhalika, Chaumma ilisema Agosti 17 na 18, sekretarieti ya chama hicho itapitia taarifa za kamati za utendaji za mikoa na kuandaa taarifa kwa Kamati Kuu ya chama.
Agosti 20 na 21, mwaka huu kitafanyika kikao cha Kamati Kuu kuandaa mapendekezo ya uteuzi wa mwisho kwa Halmashauri Kuu kwa wagombea wa nafasi za ubunge na uwakilishi wa majimbo.



