Chiki, Mafufu wakemea wageni wanaoleta uchochezi

DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji wa Filamu Tanzania, Chiki Mchoma, amewataka wageni wanaoingia nchini kwa lengo la uchochezi kuacha mara moja, akisisitiza kuwa Tanzania si nchi ya kujaribia.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Chiki amesema wamepokea salamu nyingi za mshikamano kutoka kwa vijana wazalendo wa Kenya waliounga mkono kauli ya viongozi wa Tanzania juu ya umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa.

“Tunasema shukrani kwa vijana wa Kenya na mzee wao Waziri kiongozi wa Baraza la Mawaziri nchini Kenya Musalia Mudavadi kwa kusimama kidete kuhusu haki na mwenendo wa kisheria wa kila nchi. Tusiingilie mambo ya ndani ya nchi nyingine, atakayejaribu atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Chiki.

Chiki amesema kuwa baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakijificha nyuma ya pazia la haki za binadamu huku wakihatarisha usalama wa nchi na kuvunja mahusiano mema yaliyodumu kwa muda mrefu.

“Vijana wa Kenya wamekuwa wakiwalamikia baadhi ya wanaharakati kuwa walisababisha maafa makubwa mwaka 2007 huko Kenya. Leo baadhi yao wanavuka mipaka kuja Tanzania kwa malengo kama hayo. Hatukubali,” amesema kwa msisitizo.

SOMA ZAIDI: Mafufu, Mchoma wakemea kauli za kuvuruga amani – HabariLeo

Kwa upande wake, kijana mzalendo Jimmy Mafufu amesema vijana wa Tanzania hawawezi kukaa kimya wakati watu wachache kutoka nje wanajaribu kuharibu amani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu.

“Sisi vijana tunasema bila woga tuko tayari kuilinda nchi yetu. Tanzania si shamba la bibi. Ukitaka kuja, njoo kwa amani. Ukija na uchochezi, vyombo vya usalama vitafanya kazi yake,” amesema Mafufu.

Amewaasa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa busara na uvumilivu wake licha ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza kutoka kwa baadhi ya mashirika na watu binafsi wanaotaka kuvuruga utulivu wa nchi.

“Rais wetu yuko imara, na vyombo vya usalama vinamtii. Yeyote anayepinga uongozi wake anapingana na maslahi ya Taifa. Hili halikubaliki,” ameongeza Mafufu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button