CUF yaahidi uchumi wa kisasa

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema serikali yake itajenga uchumi wa kisasa wenye ushindani kitaifa na kimataifa.
Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho imeeleza uchumi huo utahimili misukosuko ya utandawazi, utakuwa kwa kasi bila kuharibu mazingira na utanufaisha wananchi wote.
Ilani imeeleza CUF itajenga mazingira mazuri ya kuwekeza, kufanya biashara na ushirikiano wa kimataifa bila kuathiri uhuru wa Tanzania.
Chama hicho kimeahidi kuweka misingi ya utawala bora na utekelezaji wa sera utakaohakikisha uchumi unakuwa kwa asilimia 10 kila mwaka ili kufanikisha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu mwaka 2030.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itawekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu kama barabara, reli, bandari, mawasiliano, nishati, maji, elimu na afya. Hii itasaidia kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara,” imeeleza Ilani hiyo.
Mapinduzi ya kilimo
Ilani imeeleza dira ya mabadiliko ya CUF inakusudia kuanzisha mapinduzi ya kweli ya kilimo yatakayoongeza uzalishaji na tija kwa kuijenga upya sekta ya maendeleo ya viwanda.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itaweka mkakati madhubuti wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani ya nchi na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na kielektroniki,” imeeleza.
Ilani imeeleza dira ya mabadiliko ya CUF inakipa kilimo nafasi ya pekee katika mikakati ya kukuza uchumi na hivyo kuwaondolea wananchi umasikini hasa wa vijijini.
“Katika miaka mitano ijayo bajeti ya sekta ya kilimo itakayoandaliwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itakuwa kati ya asilimia 10-15 ya bajeti yote,” imeeleza.
Madini
Ilani imeeleza serikali ya CUF itahakikisha sekta ya madini inachangia asilimia 30 ya thamani ya mauzo ya madini kwenye mapato ya serikali.
Pia, imeeleza serikali ya umoja wa kitaifa ya CUF itajenga mfumo mzuri wa usimamizi na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, itaondoa misamaha holela ya kodi na itabana mianya ya ukwepaji wa kodi ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi na viwango vya kodi na tozo mbalimbali.