CUF yahimiza kupiga kura Oktoba 29

MOSHI : CHAMA cha Wananchi (CUF) kimehimiza wananchi waende kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu.
Mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Samandito Gombo alisema hayo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati wa mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Kituo Kikuu cha Mabasi katika Manispaa ya Moshi juzi. “Jitokezeni kwa wingi kwenda kupiga kura, kuichagua CUF. Usipopiga kura unadhulumu nafsi yako, unawadhulumu watoto wako, familia yako kwa ujumla na pia unaidhulumu hata nchi yako.
Usidanganywe na mtu yeyote anaekushauri usiende kupiga kura, maana huwezi kumpata kiongozi au serikali nzuri bila ya kupiga kura,” alisema Gombo. Alisema kampeni za chama hicho zimelenga kuwaelimisha wananchi sera za chama hicho zenye ajenda mahususi kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania. SOMA: Mgombea urais CUF atangaza vita wezi mali za umma
“Jambo la kwanza ambalo tunalipa kipaumbele ni kuboresha sekta ya elimu kwa kuajiri walimu wengi zaidi, kukabiliana na changamoto iliyoko sasa ya upungufu wa walimu nchini. Tuna shule nyingi lakini kila kukicha tunasikia changamoto ya upungufu wa walimu, wakati wako ambao wamehitimu lakini hawajaajiriwa,” alisema

Gombo. Pia, alisema kuna changamoto kwenye sekta ya afya na kwamba haoni sababu ya watu wakose kuajiriwa, wakati serikali inaingiza fedha nyingi kila mwaka. “Iwapo CUF tutapata ridhaa ya wananchi kuiongoza serikali inayokuja, cha kwanza ni kuhakikisha hazina inapata waajiriwa waaminifu na wenye weledi wa hali ya juu.
Kupitia kwao, matumizi ya fedha yatakuwa mazuri na kila Mtanzania anayemaliza elimu atapata ajira,” alisema Gombo. Alisema serikali ya CUF pia itafanya mabadiliko katika mfumo wa kodi utakaowezesha kuboresha makusanyo ya fedha za serikali.



