Dar, TRA kuimarisha mazingira ya kodi Kariakoo

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam ipo tayari kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuhakikisha wafanyabiashara wa soko kuu la kimataifa la Kariakoo wanapata mazingira rafiki yenye kuleta faida kwa mlipa kodi.

Mpogolo ameeleza hayo Dar es salaam katika mkutano uliofanyika kati ya viongozi wa halmashauri, Kamishna Mkuu wa TRA na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo.

Aidha, Mpogolo amezungumza juu ya mikakati waliyojiwekea na wafanyabiashara wa Kariakoo wakiwepo machinga kufanya soko ilo kuwa rafiki na mazingira yenye kuleta faida kwa mlipa kodi.

Amesema endapo wafanyabiashara watakuwa katika mazingira rafiki ya kibiashara wana uwezo wa kulipa kodi, kuliko wanavyofanya sasa katika mazingira finyu ya barabarani.

Mpogolo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya la kimataifa kariakoo, baada ya kuungua moto kwa soko la awali.

Pia Mpogolo amemuhakikishia kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda, kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano kwa jumuia ya wafanyabiashara kariakoo, pamoja na jumuia ya wafanyabiashara Dar es salaam, kwani serikali inatambua namna walivyoweza kutoa ajira kwa watu wengi na kulipa kodi.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara ambao hawamo katika umoja wajiunge ili waweze kusaidiwa kirahisi changamoto zao kupitia viongozi wao, na kunufaika na umoja huo.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amebainisha mchango mkubwa wa wafanyabiashara Kariakoo kwa kuzalisha walipa kodi wakubwa, wa kati na wadogo jambo ambalo TRA inajivunia.

Mwenda amesema mipango ni kuhakikisha umuhimu wa soko na wafanyabiashara Kariakoo kuzalisha mabilionea wazawa na si wageni kupitia soko hilo.

Nao wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamesema wako tayari kulipa kodi, ili wafanye biashara zao kwa amani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button