Daraja la Masagi kufungua fursa Iramba

SINGIDA : KUKAMILIKA kwa daraja la Masagi linalojengwa katika barabara ya Kibirigi–Masagi kunatarajiwa kuunganisha vijiji vya Kibirigi, Masagi na Tyeme katika Kata ya Mtoa, Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, na kufungua njia za mawasiliano na masoko ya mazao.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahim Kibasa, amesema daraja hilo litasaidia wakulima na wafugaji wa eneo hilo kufikia masoko kwa urahisi, baada ya muda mrefu kukwama kutokana na kukosekana kwa kivuko cha uhakika katika Mto Sekenke.

“Vijiji hivi vinajishughulisha na kilimo cha pamba, alizeti, dengu na mahindi pamoja na ufugaji. Kukosekana kwa daraja kumekuwa kikwazo kwao katika kusafirisha mazao yao na kujiendeleza kiuchumi,” alisema Kibasa.

Alieleza kuwa mradi huo, licha ya changamoto za mvua wakati wa utekelezaji, umekaribia kukamilika na utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa kata hiyo na wilaya kwa ujumla. SOMA: Kagera mambo mazuri utekelezaji miradi ya barabara

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA, CPA Ally Rashid, aliwataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha ubora wa kazi na kuyashughulikia mapungufu yaliyobainika wakati wa ukaguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button