DART yasaini mikataba kuleta mabasi 932

DAR ES SALAAM; WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), umesaini mikataba na watoa huduma binafsi kwa ajili ya kuleta mabasi mapya 932 kwa awamu ya kwanza na ya pili hadi ifikapo Oktoba mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia alisema hayo ofisini kwake Dar es Salaam jana wakati akizungumza na wanahabari.

Dk Kihamia alisema mikataba hiyo ilisainiwa na watoa huduma wanne wakiwemo watatu wa Tanzania.

Alisema mabasi hayo yataanza kuwasili nchini katikati ya Agosti mwaka huu ambapo yatapokewa mabasi 99 kabla ya mengine kuwasili nchini mwezi unaofuata na kukamilika Oktoba mwaka huu.

Alitaja kampuni hizo na mabasi yatakayoletwa katika mabano ni Mofat Company Limited (255) ya njia kuu yenye urefu wa meta 18, Metro City Link Ltd (334) ya njia za mlisho kwa njia tatu na YK City Link Ltd (166) kwa njia sita za mlisho na mabasi yote yakiwa ni kwa ajili ya barabara ya Mbagala.

Aliongeza kuwa kati ya mabasi 255 yanayoletwa na Kampuni ya Mofat, mabasi 150 tayari yamepakiwa kwenye meli na yanatarajiwa kufika Bandari ya Dar es Salaam Agosti 15, 2025.

Aidha, Dk Kihamia alisema mtoa huduma wa nne ni Kampuni ya TransDar ambayo imepewa jukumu la kuleta mabasi 177 kuchukua nafasi ya mtoa huduma wa mpito. Kampuni inaendeshwa kwa ubia kati ya Mtanzania na Kampuni kutoka Falme za Kiarabu (UAE).

Kadhalika, Dk Kihamia aliwakumbusha wadau na umma kwa ujumla kuwa Dart ndiye msimamizi pekee na msemaji halali wa wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

Alibainisha kuwa kutokana na ukweli huo, mawasiliano yoyote ya utekelezaji wa mradi, sera au mipango lazima yatoke rasmi kupitia Dart.

“Kumekuwa na taarifa zisizo sahihi zilizotolewa na baadhi ya watoa huduma binafsi zikihusisha majukumu ya usimamizi, ununuzi wa mabasi na shughuli za waendeshaji wenzao. Taarifa hizo ni batili na zinakiuka taratibu za mawasiliano zilizowekwa na Dart,” alisema Dk Kihamia.

Alisisitiza kuwa hakuna mtoa huduma anayeruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala ya kifedha, mikataba ya ununuzi wa mabasi au mipango ya waendeshaji wenzao kwani masuala hayo yapo chini ya Dart.

Katika hatua nyingine, Dk Kihamia alivikumbusha vyombo vya habari kuhakikisha vinathibitisha taarifa kwa Dart kabla ya kuzichapisha ili kuepuka upotoshaji na kwamba mawasiliano yote kwa umma kuhusu mradi wa BRT yanapaswa kuratibiwa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha Dart.

Awamu ya Kwanza ya mradi inatoka Kimara hadi Kivukoni, awamu ya pili ni kutoka Mbagala hadi Gerezani, awamu ya tatu inatoka Gongo la Mboto hadi Gerezani na ya nne inatoka Tegeta hadi Morocco.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button