DAWASA yatakiwa kupunguza upotevu wa maji

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Kudumu ya Bunge, Uwekezaji na Mitaji ya Umma imewataka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza nguvu na kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 37 ya sasa mpaka kiwango kinachopendekezwa kimataifa cha asilimia 20 ili kuboresha huduma kwa wananchi wote.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo wakati akikagua maendeleo ya mradi wa jengo jipya la DAWASA linatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na kugharimu Sh bilioni 48.9, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Deus Sangu amesema kuwa kamati imejionea utekelezaji mzuri wa mradi huo na limeridhika na ufanisi, ubora wa jengo hilo.

Mbali na hapo Mwenyekiti wa Kamati ameipongeza Mamlaka kwa kuweza kuongeza wigo wa utoaji wa huduma kutoka wateja 200,000 mpaka wateja 432,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Advertisement

Amesema kuwa kupitia jengo hilo DAWASA ambayo ni mamlaka kubwa ya maji nchini litasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Laston Msongole ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kutembelea mradi huo utakaohudumia majimbo 16 ya uchaguzi na mikoa minne ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, baadhi ya maeneo ya Morogoro na Tanga.