DC aagiza wananchi warudishiwe fedha zao

MKUU wa Wilaya ya Mpanda, Jamilla Yusuf ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya nsimbo kurudisha fedha kwa wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi katika Mto Katuma.
Ameto kauli hiyo kutokana na malalamiko ya wananchi hao waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi katika Mto Katuma uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Katavi kuomba kurudishiwa fedha zao walizotoa kwa ajili ya kukatiwa vibali vya uvuvi.
Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa akisikiliza kero za wananchi wa Kata ya Sitalike iliyopo Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi, ambapo wananchi hao wamesema wamebaini vibali walivyokatiwa havikuainisha eneo rasmi la kufanyia shughuli hiyo ya uvuvi.
Awali baada ya malalamiko hayo, Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Nsimbo Daniel Walakunga amesema vibali vilivyotolewa havikuwa na mamlaka ya kufanya shughuli za uvuvi ndani ya Hifadhi ya Taifa Katavi na badala yake shughuli hizo zifanyike maeneo yote ya halmashauri hiyo isipokuwa eneo la hifadhi.
Amesema baada ya kukinzana na wananchi hao, serikali ilifanya uamuzi wa kurudisha fedha hizo kwa wananchi, jambo ambalo wananchi walipinga kuwa halikufanyika.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya, akakata mzizi wa fitina kwa kuamrisha halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kurudisha fedha hizo kwa wananchi.



